Thursday, September 03, 2015

WAZIRI MKUU AALIKA WAWEKEZAJI KUTOKA VIETNAM



WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema wakati Tanzania inajiandaa kutekeleza awamu ya pili ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano (2016 -2020) ambao unalenga kukuza viwanda nchini, haina budi kuangalia ni aina gani ya uwekezaji unafaa kuchukuliwa kwa manufaa ya nchi.

Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumatano, Septemba 2, 2015), wakati akizungumza na mabalozi na wageni mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya miaka 70 ya Uhuru wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam na miaka 50 ya kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia baina ya Tanzania na Vietnam, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Huu ni wakati muafaka kwa nchi zetu kuangalia ni aina zipi za uwekezaji zinafaa kuchukuliwa kwa manufaa ya nchi zetu na wananchi wake. Nitumie fursa hii kuwakaribisha wawekezaji kutoka makampuni ya Ki-Vietnam waje kuwekeza kwenye usindikaji wa korosho, utengenezaji wa saruji na viwanda vya nguo,” alisema.

Aliyataja maeneo mengine ambayo wenye makampuni wanaweza kuwekeza kuwa ni nyanja ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na ujenzi wa nyumba za kuishi (real estate development).

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuipongeza kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vietnam (VIETTEL) kwa uamuzi wake wa kutenga dola za Marekani bilioni moja ambazo zitatumika kuendesha shughuli zake hapa nchini.

“Huu ni mtaji mkubwa sana, siyo tu hapa Afrika Mashariki na Kati bali hata barani Asia. Uwekezaji huu utazalisha ajira za moja kwa moja 1,700 na ajira nyingine 20,000 ambazo si za moja kwa moja,” aliongeza.

Kwa upande wake, Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Bw. Vo Thanh Nam alisema tangu ipate uhuru wake hadi, nchi hiyo imekwishaanzisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi 185 na wakati huo huo imekwishaweka mahusiano ya kibiashara na uwekezaji na nchi 220. “Vietnam ni mwanachama hai katika mashirika ya kimataifa na kikanda zaidi ya 70 yakiwemo UN, WTO, ASEAN NA APEC,” alisema.

Akizungumzia kuhusu miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya Vietnam na Tanzania, Balozi Thanh Nam alisema mbali ya kujenga mahusiano ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, nchi hizo mbili zimeunganishwa na uwekezaji uliofanywa na kampuni ya VIETTEL GROUP kwenye sekta ya mawasiliano.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Yahaya Simba na mabalozi wa nchi mbalimbali wakiongozwa na Balozi Juma Alfani Mpango, ambaye ni Mkuu wa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.



IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

No comments:

Post a Comment