Sunday, May 03, 2015

Yaliyojificha kuporomoka kwa shilingi dhidi ya Dola ya Marekani-Shilingi inahujumiwa na Mabenki?




Katika ukurasa wangu wa facebook mnamo tarehe 25 Aprili 2015 niliandika kuhusu sababu za shilingi kuporomoka thamani na majawabu ya namna ya kurejesha thamani halisi ya sarafu yetu. Nilieleza “Shilingi kuporomoka dhidi ya dola na kuvuka 1$/2000TS kunasababishwa na sababu kadhaa 1) Woga wa uchaguzi na hivyo Dola nyingi kutoingia nchini (FDI etc) kusikilizia Serikali ijayo inaundwaje 2) Woga wa uchaguzi na hivyo matajiri kununua dola kwa kasi (too many Tshs chasing too few $) ili kuzificha (hoard) nje 3) kutouza mazao nje na kuagiza bidhaa nyingi kutoka nje ( current account deficit) 4) Benki Kuu kutoachia $ nyingi kwenye soko kutokana na akiba ya fedha za kigeni kupungua 5) Kuongezeka kwa huduma ya Deni la Taifa ambapo malipo ni kwa fedha za kigeni kwa madeni yaliyo wiva.
Niliendelea kushauri majawabu “Suluhisho 1) Benki Kuu kuachia $ za kutosha kwenye soko katika muda mfupi na wa kati (Mwezi Februari BoT ilifanya hivi na kuongeza $64 milioni kwneye soko bila mafanikio[2] 2) Kuongeza mauzo nje hasa ukizingatia kwa sasa ‘our exports becomes cheaper vis a vis foreign exchange) 3) Malipo ya kodi ya Ongezeko la Mtaji kutoka BG (Shell transaction ) na Ophir (Pavilion transaction), malipo haya kwa fedha za kigeni 4) Punguza kununua vitu vya anasa kutoka nje 5) Unafuu wa huduma kwa Deni la Taifa ( Debt relief ) 6) Punguza ujazo wa fedha nchini (mop tshs out)”.
Mjadala mkali umeendelea kuhusu suala hili katika majukwaa mbali mbali. Ni dhahiri kuporomoka kwa shilingi kunaathiri sana Watanzania wa ngazi ya kati hasa wafanyabiashara wa kati wenye kununua huduma na bidhaa kutoka nje. Wenye viwanda wanaotegemea malighafi kutoka nje gharama zao za uzalishaji zimeongezeka zaidi na hivyo kuhatarisha uzalishaji mali nchini. Licha ya kwamba kuporomoka kwa shilingi kunafanya bidhaa zetu za kuuza nje kuwa rahisi, lakini huchukua muda kuzalisha bidhaa hizo na hasa kilimo kuweza kufaidika hali hiyo. Kwa hiyo ni faida kwa nchi kwa sasa kuwa na sarafu stahmilivu ( stable) iliyojengwa kwenye misingi imara ya Uchumi. Hata hivyo, inaonekana kuwa sarafu ya Tanzania inahujumiwa. Kuporomoka kwa Shilingi katika wiki za hivi karibuni sio matokeo ya nguvu za soko bali ni matokeo ya hujuma ( currency manipulations).
Mabenki makubwa ya kigeni nchini, inasemekana, katika miezi ya karibuni yamefanya currency manipulations na kupelekea dola chache kukimbizwa na shilingi nyingi na hivyo bei ya dola kupanda bei. Hii inatokana na ukweli kwamba Benki zetu kubwa tatu zinazoongoza zinaendeshwa na wageni. Inasemekana biashara hii hufanyika kati ya matawi ya Benki za kigeni hapa nchini na makao makuu yao. Kuporomoka kwa shilingi kunakotokea hivi sasa hakuendani na kuporomoka kwa miaka ya nyuma kipindi kama hiki (ambacho ki kawaida ni miezi shilingi hushuka thamani kwa sababu ya watalii kuwa wachache na mauzo ya bidhaa nje kuwa madogo sana). Wastani wa miaka 10 iliyopita inaonyesha kuwa kipindi hiki shilingi hushuka kwa kati ya 8% mpaka 13% na sio kuporomoka kwa zaidi ya 20% kulikotokea hivi sasa. Kwa mfano mwaka 2011 miezi kama hii ( Februari – Mei) Shilingi iliporomoka kutoka shs 1,380 kwa dola 1 mpaka shs 1,570 sawa na mporomoko wa 12%. Hata hivyo kuanzia mwaka huo mpaka mwaka 2014 shilingi imekuwa ikishuka thamani kwa kiwango kidogo sana. Mwaka 2013 thamani ya shilingi ilishuka kwa wastani wa asilimia 1.7 tu.
Uchambuzi huu wa thamani ya sarafu yetu unaonyesha kuwa kuna zaidi ya nguvu ya soko kunakotokana na mauzo yetu nje kuwa machache. Vile vile kupanda kwa thamani ya dola ya marekani duniani hakutoshi kuelezea mporomoko huu wa kasi wa shilingi kuanzia mwezi Disemba mwaka 2014 mpaka sasa. Tuhuma za mabenki kuwa yanahujumu shilingi (currency manipulations) zaweza kuwa na ukweli.
Vile vile, inasemekana kumekuwa na utoroshaji mkubwa wa dola kutoka nchini kwenda nje ya nchi. Utoroshaji huu unafanyika kupitia wasafiri wanaopita ukumbi wa VIP uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam. Utoroshwaji huu unatokana na hofu isiyo ya msingi kwamba uchaguzi utakuwa na vurugu. Utoroshwaji wa fedha ni kinyume sheria zetu. Sheria zetu za fedha za kigeni zinazuia mtu kubeba zaidi ya dola 10,000 za kimarekani zikiwa taslimu, kuingia nazo nchini au kutoka nazo nchini. Tafiti za haraka zinaonyesha kuwa huu umekuwa ni utaratibu wa kawaida kila mwaka wa uchaguzi tangu mfumo wa vyama vingi uanze.
Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuchukua hatua zifuatazo;
1.     Kufanya uchunguzi wa kushtukiza mara moja dhidi ya benki zote za kigeni zilizopo hapa nchini. Uchunguzi huu utazame biashara ya fedha za kigeni ya benki hizi kwa lengo la kuzuia ‘ currency manipulations’ na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Benki yeyote itakayokutwa imehujumu biashara ya fedha za kigeni kwa lengo la kushusha thamani ya shilingi dhidi ya dola za kimarekani.
2.     Jeshi la Polisi na kitengo cha kuzuia utoroshaji wa fedha ( anti money laundering unit) kufanya ukaguzi wa lazima wa watu wote wanaosafiri kwenda nje ikiwemo wanaopita sehemu ya watu mashuhuri (VIP Lounge) ili kudhibiti utoroshaji wa fedha za kigeni kwenda ughaibuni.
3.     Watanzania tufikirie upya nafasi ya Mabenki katika uchumi wa nchi na kufanya maamuzi magumu ya kurejesha baadhi ya Benki katika umiliki mpana zaidi wa Watanzania. Kwa malengo ya muda wa kati, Benki kubwa 3 nchini ilazimu kuwa na umiliki unaozidi 51% wa Watanzania. Bila ya kushika mabenki nchi itachezewa sana.
4.     Suluhiho la kudumu la sarafu stahmilivu ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kuuza nje ya nchi na kupunguza manunuzi ya bidhaa kutoka nje. Urari wa Biashara wa Tanzania umepanuka kutoka $1bn mwaka 2004 mpaka $6bn mwaka 2013 (BOT 2013) kutokana manunuzi yetu nje kukua kwa kasi kutoka $2.5bn mpaka $11bn wakati mauzo yetu nje yakikua kwa kasi ndogo kutoka $1.4bn mpaka $5bn katika kipindi hicho. Isingekuwa uimara katika urari katika uwekezaji na uhamisho wa mitaji, Tanzania ingekuwa na sarafu yenye thamani sawa na takataka. Serikali ihimize uzalishaji mali mashambani na viwandani na kuuza nje biadhaa zilizoongezwa thamani. Zama za kutegemea dhahabu zimekwisha na sio endelevu. Turudi kwenye misingi: Bidhaa za Kilimo na Viwanda.
Tutaendelea kufuatilia thamani ya shilingi mpaka ifikapo mwezi Julai ambapo ndipo kipindi kigumu kwa shilingi huwa kihistoria. Hatua zilizoainishwa zisipotazamwa na mamlaka tajwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani yaweza kufikia tshs 3000!
[1] Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo. Amepata kuwa Waziri Kivuli wa Fedha na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PAC
[2] Benki Kuu kuingiza $ kwenye soko kuna hatarisha kupunguza Akiba ya fedha za Kigeni. Kutokana na ujinai unaoendelea kwenye soko la fedha za kigeni nchini, BoT kuendelea kumwaga fedha za kigeni inaweza kuwa ni mkakati wa kudumu wa wanaofaidika na ‘currency manipulations’. Kushinikiza Benki Kuu kuendelea kubomoa foreign reserve ni kutokuona mbali na kujaribu kujiridhisha kwa kutibu dalili za ugonjwa badala ya ugonjwa wenyewe.

No comments:

Post a Comment