Friday, May 08, 2015

WATANZANIA WEKEZENI KWENYE VIWANDA - PINDA



WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda amewataka Watanzania wenye uwezo wa kifedha waangalie uwezekano wa kuanzisha viwanda hapa nchini badala ya kuendelea kuwa wachuuzi wa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi na kuziuza hapa nchini.

Ametoa wito huo jana jioni (Jumatano, Mei 6, 2015) baada ya kutembelea maonyesho ya biashara ya Syria yanayoendelea kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania pamoja na wafanyabiashara kadhaa, Waziri Mkuu Pinda alisema mtindo unaoendelea wa kuuza mazao ghafi nje ya nchi hauisaidii Tanzania kama nchi na badala yake unanemeesha viwanda na uchumi wa nchi zinazonunua mazao hayo.

“Watazania lazima wajiulize hivi bidhaa zote wanazoagiza kutoka nje ya nchi haziwezi kabisa kuzalishwa hapa nchini ili kupunguza matumizi mkubwa ya fedha za kigeni, kukuza uchumi na kuongeza ajira?,” alihoji Waziri Mkuu.

Alisema wakati umefika sasa wa Tanzania kufikiria kuanzisha mpango mahsusi wa kulinda viwanda vya ndani kwa kuweka vivutio vitakavyowashawishi wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuanzisha viwanda vitakavyotumia malighafi inayozalishwa hapa nchini hatua ambayo itawafanya wafanyabiashara wasiende nje kununua bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini.

Mapema, Balozi wa Syria nchini, Mhe. Abdulmounem Annan alimweleza Waziri Mkuu kuwa nchi yake inavyo viwanda vya nguo za pamba zaidi ya 100 na pamba ghafi yote inayotumika kwenye viwanda hivyo inalimwa nchini humo.

Balozi Anan alisema yuko tayari kuandaa utaratibu utakaowawezesha wafanyabiashara, wawekezaji na viongozi wa Serikali kwenda Syria ili kukutana na wenzao kwa lengo la kujifunza na kuwashawishi waje kuwekeza Tanzania kwenye viwanda vya nguo na vya kusindika vyakula.

(mwisho)

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,

No comments:

Post a Comment