Tuesday, April 21, 2015

WATANZANIA WALIOKO NJE WASHAURIWA KUHAMISHA MITAJI YAO KWA KUWEKEZA NCHINI, PASKAZIA BALONGO ANASIMULIA



NA AUDAX MUTIGANZI, BUKOBA +255 784 935 586

Uwekezaji  katika nchi hii ni sera iliyotiliwa mkazo na rais wa jamhuri ya muungani wa Tanzania wa awamu ya tatu, Benjamini William Mkapa, sera hii imechangia kuchochea kasi ya maendeleo kwa kuleta mabadiliko katika  nyanja za  kijamii na kiuchumi.

Ninachotaka kusema  sera ya uwekezaji imechangia kuboresha na kuimarisha huduma katika Nyanja mbalimbali ndani ya jamii, imeongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani, imekuza  sekta ya utalii, imeboresha masuala ya kilimo mambo ambayo yanachangia ukuaji wa pato la taifa.

Ni lazima tukubali kwamba sera hii imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ukosefu wa ajira hasa kwa wanaohitimu masomo yao katika ngazi mbalimbali hapa nchini walikokuwa wakitegemea sana ajira zinazotolewa na serikali ambazo ni chache  ukilinganisha na idadi ya wanafunzi wanaohitimu masomo yao katika vyuo  vya elimu ya juu na elimu ya kati.

Kwa  maana hiyo hatuna budi kumpongeza rais mstaafu wa awamu ya tatu, kwa kutilia  mkazo  suala la uwekezaji, katika kutilia mkazo suala la uwekezaji  aliweka mazingira mazuri  ambayo hadi sasa yanaendelea kuwavutia wale wanaojitokeza kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali.

Ndugu zangu Watanzania  ni lazima tukubali kwamba mchango wa Rais Mstaafu Mkapa katika kuendeleza nchi hii ni  mkubwa,  sera ya uwekezaji imechangia kwa kiasi kikubwa matumizi ya rasilimali zilizo adimu zinazopatikana  hapa nchini ambazo  ni pamoja na malighafi zinazotumiwa na viwanda vya wawekezaji vilivyoko hapa nchini vinavyozalisha bidhaa mbalimbali.

Ni kweli sera hii ni nzuri imechangia kuchochea kasi ya maendeleo, katika utafiti wangu nilichokigundua ni kwamba wawekezaji  walio wengi wanaojitokeza kuwekeza hapa nchini ni wale wanaotoka nje ya nchi.

Kwa uelewa nilikuwa nao ni wawekezaji wachache toka nje ya nchi ambao wanaweza kuwa na machungu ya nchi hii katika kuhakikisha  inapiga hatua kubwa kimaendeleo.
 Ninachokielewa kila mwekezaji anayejitiokeza kuwekeza hapa nchini lengo lake kubwa ni kuchuma mali na kuondoka bila kutangulizambele maslahi ya nchi, hakuna mwekezaji ambaye anaweza kuwa na machungu ya nchi hii bila kutanguliza maslahi yake binafsi kwa kuwa anawekeza kwa lengo la kupanua myaji wake ndio maana wawekezaji wanajitokeza wanakuja kibiashara zaidi.

Je, sisi Watanzania wenye uwezo tulioko ndani na nje ya nchi tuko wapi? Ni lazima tujiulize swali hilo kwa kuwa ni la ufahamu, kinachonishangaza na kuniuma ni pale ninapowaona baadhi ya Watanzania wenye mitaji mikubwa  wakosa moyo wa uzalendo hasa pale wanapofikia  katika mataifa mengine.

Kuna usemi ‘usemao samaki mmoja akioza sio kwamba wote wameoza’  usemi huu nitakubaliana nao sio kwamba watanzania wote waishio nje ya nchi wenye mitaji mikubwa wanaokosa moyo wa uzalendo, kuna baadhi ya Watanzania  wanaokumbuka walikotoka  kwa kutenga mitaji walionayo kwa kuwekeza hapa nchini.

Miongoni mwa Watanzania waliotenga sehemu ya mitaji waliyo na hatimaye kuwekeza nchini ni pamoja na Paskazia Barongo Mtanzania aishiye nchini Sweeden ambaye amejitokeza na kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuanzisha chuo cha ualimu kinachojulikana kwa jina la ERA kilichoko katika mtaa wa Kagemu ulioko katika kata ya Kitendagulo, mkoani Kagera.

Chuo hicho kinatoa mafunzo ya ualimu daraja la tatu ngazi ya cheti, Bi Balongo anasema  kwamba chuo hicho kimeanza rasmi kutoa mafunzo ya ualimu kuanzia mwaka jana mwezi wa nane, anaeleza kwamba  alifikiria mpango wa kuanzisha chuo hicho  mwaka 2008 baada ya kupona katika ajali mbaya sana ya gari aliyoipata akiwa nchini Sweeden.

Anaeleza kwamba baada ya kupona katika ajali hiyo alijisikia kwamba ana deni kubwa kwa watanzania hususani wazaliwa wa mkoa wa Kagera hasa waliomuombea hadi akafikia hatua ya kupona, anasema kuwa katika ajali alivunjika vunjika sehemu mbalimbali za viungo vya  mwili wake.

Bi. Barongo anasema katika kuwaenzi Watanzania walimuombea hadi akapona baada ya ajali hiyo alilazimika kuwekeza katika sekta ya elimu na sekta ya afya, anasema amelazimika kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuwa inamchango mkubwa katika ustawi ndani ya jamii.

Anasema kuwa anachokiamini ni  kwamba kama waliompatia matibabu hadi akapona  wasingekuwa na elimu wasingefanya chochote kulingana na hali mbaya aliyokuwa nayo baada ya kupata ajali hiyo, anaendelea kusema kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha pamoja na kukabiliwa na changamoto nyingi.

Anabainisha kwamba hakulazimika kuwekeza katika sekta ya elimu kwa lengo la kufanya biashara bali amewekeza katika sekta hiyo kwa lengo la kutoa huduma, katika kutoa huduma anasema kwamba chuo chake kinampokea mwanafunzi yoyote aliyemaliza kidato cha nne bila kujali ufaulu wake.

Bi. Balongo anasema wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wenye ufaulu mzuri  wanajiunga moja kwa moja na mafunzo  ya cheti cha ualimu ngazi ya daraja la tatu na wale wanaojiunga na chuo hicho wenye ufaulu usioridhisha wanapatiwa elimu maalumu ya kuwawezesha kurudia mitihani yao inayowapa sifa ya kufanya mitihani ya cheti cha ualimu.

Anaendelea kusema kuwa chuo chake kinatoa elimu ya kiwango cha juu ambayo inaenda sambamba na vyuo vya ualimu vinavyomilikiwa na serikali, anasema kuwa ataendelea kukiboresha chuo hicho , anasema kuanzia mwaka kesho chuo hicho kitaanza kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya kilimo.

Bi. Barongo anasema  chuo kimelazimika kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya kilimo kwa lengo la kuwawezesha vijana waweze kujiari wenyewe  na ili waachane na dhana ya kutegemea ajira chache zinazotolewa na serikali.

Amesema  mafunzo yatakayotolewa kwa vijana yatawawezesha kujifunza mbinu bora za kilimo, anabainisha kuwa kilimo kinalipa vizuri ukilinganisha na shughuli nyingine za uzalishaji mali zinazohitaji mitaji mikubwa.

“ Nina mpango mkubwa wenye lengo la kuboresha maisha ya vijana, mimi sikuwekeza kwa leng la kupata faida nimewekeza katika sekta ya elimu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi na ndio maana najitolea katika mambo mengi, mimi ni tofauti na wawekezaji wengine wanaotafuta faida” anasema.

Bi.Barongo anasena chuo chake cha ERA kina eneo kubwa ambalo litawawezesha wanafunzi watakaojitokeza kusoma masuala ya kilimo kujifunza kwa vitendo badala ya kupata mafunzo ya masuala ya kilimo kwa njia ya vitabu.

Anasema chuo kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 129 na matarajio ya chuo hicho ni kupokea   wanafunzi 500 kwa wakati mmoja pindi miundo mbinu itakapokamilika, akielezea miundo mbinu ya chuo anasema kwa sasa chuo hicho kina jumla ya mabweni mawili ya wasichana na moja la wavulana.

Akielezea miundo mbinu mingine katika chuo hicho anasema kina madarasa matatu , chumba cha walimu, maktaba dogo, chumba cha komputa, ofisi ya walimu, ofisi ya mkurugenzi na ofisi ya makamu mkuu wa shule na jiko la kisasa, anaongeza kuwa chuo hicho kwa sasa kinatoa ajira kwa watu 26.

Katika kueleza changamoto mbalimbali zinazokikabili utendaji wa kazi wa chuo hicho Bi.Barongo anasema utaratibu wa serikali kubadili mifumo yake mara kwa mara kwamba inaathiri kiwango cha elimu.

Akitoa ufafanuzi wa changamoto hiyo  anaeleza kwamba chuo hicho kwa mara ya kwanza kilisajiliwa na wizara ya elimu, anasema kwa sasa vyuo vyote binafsi vinatakiwa kusajiliwa NACTE,  anaendelea kusema kuwa ubadilishwaji wa mfumo wa usajili wa vyuo kwamba unavigharimu na unawavunja moyo wawekezaji katika sekta ya elimu.

Ameishauri serikali  kuboresha zaidi  manzingira ya uwekezaji katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha inazishawishi taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wawezekazi katika sekta ya elimu yenye riba na masharti nafuu, tofauti riba inayotozwa kwa wawekezaji katika sekta nyingine zinazojihusisha na masuala ya biashara ya moja kwa moja.

Pia ameishauri serikali kuondoa ukilitimba katika zoezi la usajili wa  mashule na vyuo vya elimu kwa kuwapa madiwani wa manispaa, majiji na halmashauri za wilaya madaraka makubwa ya kutoa vibali vya uanzishwaji wa mashule na vyuo.

Bi.Barongo anasema kwa kiasi Fulani mgogoro katika manispaa ya Bukoba ambao ulipelekea kutofanyika kwa vikao vya baraza la madiwani  kwamba ulimuathiri sana kwa kuwa ulimchelewesha upatikanaji wa kibali cha kuanzisha chuo hicho hali iliyomgharimu sana kwa kuwa alikuwa analazimika kuja nchini mara kwa mara kufuatilia usajili.

Anamalizia kwa kuwapongeza wale wote waliomtia moyo hadi akatimiza adhima yake ya ya kuanzisha chuo cha ualimu, pia amewahimiza Watanzania kukumbuka walikotoka  kwa kutenga mitaji waliyonayo na kuwekeza hapa nchini kwa kuwa Watanzania ndio wenye uchungu na nchi yao.

No comments:

Post a Comment