Sunday, April 12, 2015

MUELEWE MKUU WA MKOA WA ZAMANI WA KAGERA KANALI MSTAAFU FABIAN MASSAWE



Tangu uhuru  wa iliyokuwa Tanganyika sasa Tanzania  mwaka 1961 miaka 53 ya uhuru mkoa wa Kagera umekuwa ukiongozwa na viongozi mbalimbali hasa katika nafasi ya  ukuu wa mkoa na kwa kipindi hicho chote hadi sasa tayari mkoa umeongozwa na wakuu wa mikoa wapatao 21 kwa vipndi  tofauti.
Viongozi hao  (Wakuu wa Mkoa)  waliowahi kuuongoza mkoa wa Kagera kwa nyakati  tofauti  waliweza kuisogeza Kagera kutoka katika hali fulani na kupiga hatua kimaendeleo katika nyanja  mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchumi, elimu,  siasa, utamaduni, miundombinu, na nyanja mbalimbali za ustawi wa jamii.
Mkoa wa Kagera chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa sasa Mheshimiwa John V.K. Mongella ulimuaga aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Kagera wa 20 na aliuongoza  mkoa  kwa miaka mitatu akiteuliwa kutoka katikanafasi ya Ukuu wa Wilaya ya Karagwe naye ni Kanali Mstaafu Fabian Inyasi Massawe kwa jina maarufu Mulokozi.
Kama walivyokuwa watangulizi wake Mhe. Kanali Mstaafu Massawe alifanya mengi katika mkoa wa Kagera na kuweka rekodi ya mambo mengi aliyoyafanya yakiongozwa na kaulimbiu yake ya “Amani na Maendeleo” kubakia katika kumbukumbu za mkoa wa Kagera na wananchi wake kwa ujumla.
Historia Fupi
Kanali Mstaafu Fabian Inyasi Massawe kabla ya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera alifanya kazi mbalimbali na mahali pengi akiwa na uzoefu mkubwa  wa uendeshaji na usimamiaji wa shughuli za umma. Kabla ya kuwa mwanasiasa amekuwa ni  Afisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania, Mtaaluma na Mwanamichezo.
Alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania mwaka 1979 katika cheo cha Luteni Usu na aliendelea kupandishwa vyeo mpaka cheo cha Kanali alichotunukiwa Januari 2002. Akiwa Jeshini alihudhuria mafunzo lukuki hadi yale ya High Commander Defence Styles.
Kitaaluma Mhe. Massawe ni Mwalimu na Mtaalamu wa Maendeleo (Development Studies).  Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni  Julai 2006, akiwa mtumishi wa umma mwenye uzoefu mkubwa hasa katika elimu ambapo alikuwa Mkuu wa shule maarufu ya Jitegemee ya Jijini Dar es Salaam  kwa muda wa miaka 17.
Kwa upande wa michezo Mhe. Massawe ni hazina kubwa ya uendeshaji na usimamizi wa michezo, aidha aliwahi kuwa Mkurugenzi wa michezo katika Jeshi la kujenga Taifa, Katibu Mkuu Tanzania Boxing Association, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Olympiki Kanda ya Tano na Mjumbe wa Balaza la Michezo Tanzania .
Medali Alizowahi Kutunzwa
Massawe aliwahi kutunzwa medali 8 (nane) za utambuzi kutokana na mchango wake uliotukuka katika utumishi wa umma. Kwanza, Octoba 1995 Wizara ya Elimu ilimtunuku cheti cha kuwa Mkuu wa shule bora. Pili, Octoba 1998 alitunukiwa cheti maalum cha utambuzi  wa mchango wake uliotukuka (Excellent contribution) katika  kukuza Uskauti nchini kutoka Skauti Tanzania.
Medali ya tatu, Januari 2002 alipewa hati ya kuutambua mchango wake katika kukuza mchezo wa handball Afrika Mashariki na Kati. Nne, Januari 2005 alipewa hati na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (East African Cooperation) katika kutambua mchango wake mahiri akiwa kiongozi wa timu ya Jeshi la Wananchi Tanzania katika mashindano ya kwanza ya michezo na utamaduni ya Majeshi ya Ulinzi ya Afrika Mashariki mjini Kampala Uganda.
Julai 2011 Mhe. Massawe alipata cheti  kutoka Bodi ya Kahawa Tanzania kwa mchango wake mkubwa  katika  kudhibiti magendo ya kahawa katika Wilaya ya Karagwe. Sita, Machi 2011 Halmashauri ya wilaya ya  Karagwe ilimtunuku cheti maalum kwa kuongoza mafanikio makubwa ya mapambano dhidi ya mimba kwa wananfunzi  na Octoba 2011 alipata zawadi kutoka Chuo Kikuu cha JohnsHopkins cha  nchini Marekani kwa kumlinda mtoto wa kike.
Utumishi wa Umma Kama Mkuu wa Mkoa
Chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa Mhe. Massawe mkoa uliendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu na aliuacha mkoa ukiwa wenye amani uhakika wa chakula. Pato la mwananchi lilikuwa shilingi 409,822/- mwaka 2011 aidha aliacha pato hilo  likiwa shilingi 716,209/- mwaka 2014
Katika kipindi chake alisimamia mkoa katika usafi na kutunza mazingira ambapo wananchi wa Manispaa ya Bukoba waliipa siku ya Alhamisi kuwa Massawe Day.  Katika Sekretarieti ya Mkoa Mhe. Massawe alihimiza mambo makuu muhimu yafuatayo:
Amani na na Maendeleo katika mkoa, alikuwa mstari wa mbele katika kupigana vita dhidi ya maadui 14 ambao ni Malumbano ya kisiasa, Uhamiaji haramu, Wizi wa kutumia siraha, Mauaji ya albino na vikongwe, Uchukuaji wa sheria mkononi, Unyanyasaji wa kijinsia, Migogoro ya ardhi na Wizi wa mifugo.
Maadui aliopambana nao Mhe. Massawe ni pamoja na Biashara ya magendo ya kahawa, Upachikaji wa mimba kwa watoto wa shule, Ushirikina na upigaji wa ramli za kichonganishi, Uharibifu wa mazingira na uchomaji moto ovyo,  Uzururaji ovyo na ukaaji vijiwni na kunywa kahawa muda wote wa kazi na unywaji wa pombe saa za kazi.
Mhe. Massawe alihimiza wananchi kufanya kazi na alijenga serikali ya mkoa yenye kushirikiana na wananchi, mashirika yasiyokuwa ya serikali madhehebu ya dini pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika mkoa na nje ya mkoa wa Kagera.
Aidha aliwahimiza wananchi kupendana na kufanya kazi na kuondokana na Kamunobele, Olwango, Kitandugaho, Etima, Obunafu na Eilangira. Hiyo yote ilikuwa ni kuchochea maendeleo na ustawi wa mkoa wa Kagera ambao upo katika kitovu cha nchi za Afrika Mashariki.
Mhe. Massawe akiwa Kagera alisimamia na kuongoza matukio matukio makubwa ya kitaifa mkoani Kagera, Kwanza mwaka 2011 Maadhimisho ya Kitaifa ya wiki nenda kwa usalaama barabarani, Miaka 50 ya uhuru Tanzania Bara. Mwaka 2012 Maandalizi ya sensa na makazi ya watu
Mwaka  2013 Mhe. Massawe alisimamia Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Kitaifa mkoani Kagera, Mchakato wa wananchi kutoa maoni ya katiba mpya, Maadhimisho ya kitaifa ya Fimbo Nyeupe, Uendeshaji wa Operesheni Kimbunga. Mwaka 2014 Uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa rekodi kubwa ya maandalizi.
Mhe. Massawe amekuwa na uhusiano na mkoa wa Kagera kwa miaka 37 na mara ya kwanza alifika Kagera akiwa Luteni wa Jeshi la wananchi wakati wa vita vya Nduli Iddi Amini. Aprili 2009 Mhe. Massawe Akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni alihamishiwa Wilayani Muleba na kuweka rekodi ya kuwa  Mkuu wa Wilaya hiyo kwa siku moja na baadae alihamishiwa katika Wilaya ya Karagwe hadi Septemba 2011 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.


ORODHA YA WAKUU WA MKOA WA KAGERA TANGU UHURU MWAKA 1961
Na.
JINA LA MKUU WA MKOA
MWAKA
1.
BW. SAMWEL N. LWANGISA
1961 - 1964
2.
BW. OSWARD MARWA
1964 - 1966
3.
Bw. P. C. WALWA
1966 - 1967
4.
BW. P. C. SEMSHANGA
1967 - 1970
5.
BW. L. N. SIJAONA
1970 -1972
6.
Maj. Gen. TWALIPO
1972 -1974
7.
Brig. M. M. MARWA
1974 -1975
8.
Col. T. A. SIMBA
1975 -1977
9.
Bw. MOHAMED KISOKI
1977 -1978
10.
Capt. PETER KAFANABO
1978 - 1981
11.
Lt. Col. NSA KAISI
1981 -1987
12.
Bw. HORACE KOLIMBA
1987 - 1989
13.
Bw. PAUL KIMITI
1989 - 1991
14.
Capt. A. M. KIWANUKA
1991 - 1993
15.
Bw. PHILIP J. MANGULA
1993 - 1996
16.
Bw. MOHAMMED A. BABU
1996 - 1999
17.
Gen. T. N. KIWELU
1999 - 2006
18.
Col. E. MFURU
2006 - 2009
19.
Bw. MOHAMMED A. BABU
2009 - 2011
20.
Col. (Mstaafu) FABIAN I. MASSAWE
2011 - 2014
21.
Bw. JOHN V.K. MONGELLA
     2014 -

No comments:

Post a Comment