Saturday, February 21, 2015

SERIKALI KUAJIRI WALIMU 35,000 - WAZIRI MKUU



WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imepanga kuajiri walimu
zaidi ya 35,000 kwa ajili ya shule za sekondari ili kukabiliana na
tatizo la uhaba wa walimu nchini.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Februari 19, 2015) wakati
akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Kiwere, mara baada ya
kukagua ujenzi wa maabara na kuzindua nyumba nne za walimu kwenye
shule ya sekondari ya Kiwere, tarafa ya Kalenga, wilayani Iringa.

Waziri Mkuu alisema walimu hao watagawanywa kwenye shule kulingana na
mahitaji yaliyokwishawasilishwa na kwamba watakapopata mgao wao hawana
budi kuziangalia kwanza shule zenye miundombinu iliyokamilika kama
ilivyo kwa shule hiyo.

Akifafanua kuhusu kasi ya ujenzi wa maabara Waziri Mkuu alisema: “Mkoa
mzima wa Iringa unahitaji kuwa na maabara 318 na zilizo tayari mpaka
sasa ni 108. Lakini kuna nyingine 141 ambazo zimekwishaanza kujengwa
na zimefikia hatua nzuri. Nimeambiwa katika muda mfupi ujao kutakuwa
na maabara 249 zilizokamilika,” alisema.

“RC inabidi uwasukume watu wako ili hizi 69 ambazo bado hazijaanza
kujengwa zikamilike kabla ya Juni mwaka huu kama ambavyo Mheshimiwa
Rais Jakaya Kikwete alikuwa ameelekeza. Alisema hataongeza tena muda
wa ujenzi,” aliongeza.

Alisema elimu ni sekta ya msingi ambayo Serikali imeamua kuipa umuhimu
wa kipekee na kuiweka katika moja ya maeneo sita muhimu ya kipaumbele
chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa ya Haraka (BRN).

Waziri Mkuu aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wasome kwa bidii na wawe
wasikivu ili waweze kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.

Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Afisa Elimu wa Wilaya ya
Iringa, Bw. Leonard Msigwa alisema ujenzi wa nyumba hizo nne ambazo
zina pande mbili (four duplex houses) umegharimu sh. milioni 323.2.
Alisema nyumba hizo zenye vyumba vitatu vya kulala, sebule na jiko,
zina uwezo wa kubeba familia nane.

Bw. Msigwa alisema ujenzi wa nyumba ulifanywa shirika la DESWOS la
Ujerumani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja
na wananchi. Pia walisaidiwa kujengewa tenki la maji na mabweni mawili
yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 112 kila moja kwa ajili ya
wasichana.

Akifafanua kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, Afisa Elimu huyo alisema
hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya Kemia na Baiolojia
lakini bado viko kwenye hatua ya kupaka rangi. Alisema mfumo wa gesi
na maji umekwishafungwa ndani ya vyumba vya maabara.

“Ujenzi wa maabara hadi sasa umekwishagharimu sh. milioni 52.8/- na
katika kipindi cha Februari 2015, tumefanikiwa kutengeneza baadhi ya
samani za maabara yaani meza 24 na stuli 96 zenye thamani ya sh.
8,940,000/-,” alisema.

No comments:

Post a Comment