Monday, August 25, 2014

MUHONGO ni MUHANGA wa propaganda ya UDINI.

Kumekuwepo na habari ambazo zimeendelea kushamiri kila uchao katika mitandao ya kijamii na pia habari hizo kuripotiwa na magazeti kadhaa, ambapo kwa mara ya kwanza gazeti la mtanzania la Jumanne ya tarehe 19th Aug 2014, kisha gazeti la Jambo leo la Alhamis ya tarehe 21stAug 2014 na baadae gazeti la An nuur la Ijumaa ya tarehe 22nd Aug 2014, kwa mfululizo, kwa mfanano wa dhamira na maandishi magazeti hayo yote yameandika habari ya upotoshaji, uchonganishi na kukuza chuki ya kidini hapa nchini. Habari katika magazeti hayo zimebeba hoja kuu UDINI wa PROF MUHONGO ambae ni Waziri wa Nishati na Madini wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo vyombo hivyo vya habari vimeripoti “unbalanced story” kuwa miongoni mwa wanafunzi 10 waliopewa scholarship na Serikali ya China hivi karibuni wote ni wakristo, na kwamba jambo hilo limefanywa kimkakati hili kuwatenga, kuwabagua na kuwakandamiza waislamu wa Nchi HII.


Ukweli halisi ni kuwa jumla ya Scholarship za Msc Oil/Gas ambazo zimetolewa katika chuo cha Petroleum nchini china ni 15 ambapo katika hizo 10 zinalipiwa na Serikali ya China na 5 zinalipiwa na Serikali ya Tanzania chini ya Wizara ya Nishati na Madini. Katika nafasi hizo 15 kwa ujumla wake, waislamu ni watano (5) na wakristo ni (10) na kigezo kikubwa kilichotumika kupata wanafunzi ni ufaulu wao katika masomo yao ya shahada ya kwanza. Miongoni wa wanafunzi watano waislamu ni A. Athuman, Swalehe L, Salum S, Hijira Yassin na Salum J.

Mtandao wa wanahabari ambao wanatumika kusambaza taarifa za upotoshaji huu pamoja na wanaowatuma wanaodhani kuwa kueneza propaganda yenye sura na taswira ya UDINI ni kumchafua Mhe Prof Muhongo na Wizara yake wamekosa ufikiri sahihi, bali kufanya hivyo kunatishia amani na mshikamano uliokuwepo baina ya watanzania. Hivyo wanaoendeleza propaganda hizo chafu ni maadui wa amani ya Taifa.

Ni ukweli ulio bayana kuwa kutokana na misimamo ya Mhe Waziri ya kusimamia haki na kupambana na ufisadi, ulaghai na ubadhirifu wa aina mbalimbali ambao ulikuwa ukifanyika katika mashirika mbalimbali yaliyo chini ya wizara yake, umeundwa mtandao hatari wa kumkabili na kuhakikisha kuwa “wanamshughilikia”. Mtandao ambao unaundwa na baadhi ya matajiri wakubwa, wanasiasa, wanasheria na wanahabari.

Ni vyema watanzania wakafahamu kuwa Wizara ya Nishati na Madini chini ya Profesa Muhongo imepata mafanikio makubwa ambapo katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya mwaka 2025, inakadiriwa kuwa Tanzania itakuwa na uchumi wa kati unaokuwa kwa asilimia 10% na kwamba matumizi ya nishati ya Umeme kwa watanzania yatakuwa zaidi ya asilimia 75%. Mafuta na gesi inategemewa kuwa ndio uti wa mgongo wa Tanzania, na misingi hiyo inawekwa sasa na Mheshimiwa Muhongo, tayari mashirika ya Wizara hiyo yameanza kuonyesha matumaini kwa kupata mafanikio makubwa na kumaliza migogoro, kesi na ubadhirifu uliokuwa ukiendelea. Uzalishaji katika migodi na madini umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa Serikali, kampuni Tanzu ya STAMICO (Shirika la Umma) ya STAMIGOLD imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa mpaka sasa.


Watanzania tunapaswa kumuunga mkono Prof Muhongo katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo watanzania. Na kwa pamoja tuiunge mkono kauli kuwa “..Tutavuka tukiwa na ushindi wa maskini na wanyonge wa nchi hii. Tutaendelea kujenga uchumi imara utakaotoa ajira na matumaini mapya kwa watanzania..”

Mungu Ibariki Tanzania.

No comments:

Post a Comment