Tuesday, March 25, 2014

HALMASHAURI YA WILAYA YA MISENYI YAWANUFAISHA WATOTO WAISHIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU



Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera imetumia jumla ya Sh.milioni 48,000,900/= kuhudumia watoto mbalimbali waishio kwenye mazingira hataraishi kwenye Halmashauri hii katika kipindi cha mwaka miaka mitatu iliyopita.

Mratibu wa Ukimwi wa Halmashauri ya Wilaya Missenyi, Rwegerera Katabaro alisema hayo mjini hapa kuwa kiasi hicho cha fedha kilitumika kuwalipia karo na kuwanunulia vifaa vya kuandikia wanafunzi 2700 wanaosoma shule mbalimbali za msingi na sekondari katika Halmashauri hii.

Akizungumzia tatizo la watoto kuishi katika mazingira hatarishi, Katabaro alisema baadhi yao wanatoka kwenye familia maskini sana, wachache ni yatima wakati wengine wametelekezwa tu na wazazi wao; hivyo kulazimika kuishi na bibi zao wasio na uwezo.

Kutokana na hali ngumu ya maisha, walezi hao huwashawishi watoto hao kujiingiza kwenye shughuli za vibarua kwa lengo la kuzisaidia familia zao kimaisha.

‘’Baadhi ya watoto hawa ulazimika kufanya vibarua katika mashamba au kujiajiri kwa kuendesha baiskeli kwa kubeba abiria maarufu kama Asecdo’’ alisema Katabaro.

Aidha, Katabaro alieleza kuwa Idara hiyo inakusudia kuimarisha Kamati za kumlinda mtoto katika ngazi mbalimbali na kuwaagiza watendaji wa kata na vijiji kuwatambua watoto wote waishio kwenye mazingira hatarishi au mazingira magumuu katika maeneo yao ili waweze kufuatiliwa.

Kwa mujibu wa Ofisa huyo, Halmashauri ya Wilaya ina jumla ya watoto 5036 waishio katika mazingira magumu, na jumla ya watoto 900 kati yao wanahudumiwa na Halmashauri kwa mwaka, hata hivyo   asasi  zisizo za serikali au za kidini nazo zinatoa mchango mkubwa katika kuwasaidia wanaobaki.

Alisema jamii inawajibu wa kuangalia namna bora ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwani watoto wa leo ni taifa la kesho, kuachana na tamaduni za kusaidia wakati wa raha
“Jamii ni lazima ibadilike na kuachana na huu utamaduni wa kuchangia katika sherehe tu bali moyo huo utumike  namna ya kuwasaidia watoto hawa’’ alisema Katabaro.

Hata hivyo alisema ili kupunguza athari zitokanazo na janga la UKIMWI  Halmashauri imeandaa mkakati malum kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ili ifikapo mwaka 2017 athari zitokanazo na janga la Ukimwi zipungue hadi asilimia 30.

No comments:

Post a Comment