Saturday, March 01, 2014

HALI YA HEWA



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA MACHI HADI MEI 2014
Taarifa hii inatoa tathmini ya msimu wa mvua za Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2013, mvua zinazoendelea katika maeneo ya kanda ya kati, magharibi, nyanda za juu kusini magharibi na mikoa ya kusini pamoja na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua za Masika katika kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei (MAM) 2014.

A.        MUHTASARI
Tathmini ya mvua za Vuli katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2013 inaonesha kuwa maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani  isipokuwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani na kanda ya kati ambayo yalipata mvua za chini ya wastani. Kwa ujumla, mtawanyiko wa mvua hizo haukuwa mzuri hasa kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua. Katika kipindi cha miezi ya Januari hadi Februari, 2014 matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile  mvua kubwa na upepo mkali yalijitokeza kama ilivyotarajiwa. Matukio hayo yalisababisha  uharibifu wa mali, miundombinu pamoja na vifo. Mtawanyiko wa mvua katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa ujumla ulikuwa wa kuridhisha. Aidha, kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua, kulikuwa na vipindi vya mvua za nje ya msimu zilizosababisha madhara mbalimbali.

Mwelekeo wa msimu wa mvua za Machi hadi Mei, 2014 unaonyesha kwamba  maeneo mengi yanayopata misimu miwili  ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu Kaskazini Mashariki na Pwani ya Kaskazini) yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini (Mikoa ya Tanga, Pwani na Dar es salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani. Mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (magharibi, nyanda za juu kusini magharibi na kusini) zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Viashiria  vikuu  vinavyotarajiwa kusababisha mvua za Masika, 2014 (Machi hadi Mei) ni kuwepo kwa joto la chini ya wastani katika eneo la mashariki mwa  Bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola) ambalo linatarajiwa kuwepo kwa kipindi chote cha msimu, joto la wastani hadi juu ya wastani katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya  Hindi na kuwepo kwa upepo wenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo kuelekea nchini hususan katika kipindi cha miezi ya Aprili na Mei, 2014. Aidha, hali ya joto katika eneo la ncha ya kusini mwa Bara la Afrika inatarajiwa kudhoofisha mfumo wa mgandamizo mkubwa wa hewa kusini mwa bara la Afrika hivyo kusababisha upungufu wa mvua za msimu wa masika katika maeneo ya ukanda wa Pwani.

B: TATHMINI YA MVUA ZA VULI OKTOBA HADI DISEMBA, 2013

Mvua za vuli katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba 2013, zilikuwa za wastani katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo ya kati mwa nchi yalipata mvua za chini ya wastani. Kwa ujumla mtawanyiko wa mvua za msimu wa Vuli  haukuwa wa kuridhisha hususan kwa maeneo mengi yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka (Tanga, Arusha na Kilimanjaro). Mvua zinazoendelea katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua zimekuwa ni za  wastani hadi juu ya wastani kwa maeneo yaliyo mengi. Aidha, maeneo mengi yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Pwani, Dar es Salaam pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro) yamepata mvua kubwa nje ya msimu kwa kipindi cha miezi ya Januari na Februari 2014. Mvua hizi za nje ya msimu zilizoambatana  na matukio ya upepo mkali na mawimbi makubwa baharini, zilisababisha madhara kama vile  vifo, uharibifu wa miundombinu na mali kwa baadhi ya maeneo. Maeneo yaliyoathirika na mvua hizo ni pamoja maeneo ya wilaya za Same, Mwanga na Hai katika mkoa wa Kilimanjaro, pia katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Morogoro ambako mafuriko yalisababisha vifo na uharibifu wa miundombinu ya barabara na Reli. Vifuatavyo ni viwango vya mvua ilivyonyesha pamoja na ulinganifu wake kwa wastani wa muda mrefu katika asilimia kwa baadhi ya vituo nchini:

Maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka:

Pwani ya Kaskazini: Matangatuani 390.1 mm (81%), Pemba 159.4 mm (57.9%), Amani 573.9 mm (110.9%), JNIA 184.6 mm (59.0%),  Zanzibar 338.9 mm (53.2%) na Morogoro 151.3mm (77.0%) za mvua.

Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki: Moshi 124.6 mm (89.4%), Arusha 222.8 mm (103.1%), Lyamungo 195.9 mm (91.8%), Same 130.0 mm (78.6%) and KIA 129.3 mm (118.3%) za mvua.

Kanda ya Ziwa Viktoria: Mwanza 365.4 mm (95.8%), Bukoba 501.5 mm (90.4%), Musoma 154.4 mm (63.4%) and Shinyanga 274.7 mm (93.9%) za mvua.

Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:

Magharibi: Tabora 394.3 mm (115.2%), Kibondo 369.4 mm (92.5%), Tumbi 361.8 mm (107.5%) and Kigoma 440.3 mm (113.7%) za mvua.

Kanda ya Kati: Dodoma 88.5 mm (58.4%), Hombolo 68.2 mm (40.7%) and Singida 135.3 mm (63.9%) za mvua.

Nyanda za Juu Kusini Magharibi: Iringa 77.9 mm (53.0%), Mbeya 228.2 mm (87.5%), Tukuyu 386.7 mm (87.1%), Sumbawanga 273.0 mm (91.0%), Mahenge 536.3 mm (109.1%) and Igeri 345.4 mm (104.9%) za mvua.

Maeneo ya Kusini: Mtwara 149.8 mm (62.9%), Naliendele 117.8 mm (43.6%)  Kilwa 58.6 mm (24.6%) and Songea 298.2 mm (124.7%) za mvua.

Angalizo: Viwango vya mvua chini ya asilimia 75 ya wastani kwa kipindi kirefu hutafsiriwa kama chini ya wastani; asilimia 75 hadi 125 hutafsiriwa kama mvua za wastani na vile vya zaidi ya asilimia 125 hutafsiriwa kama juu ya wastani.

C: MWELEKEO WA MIFUMO YA HALI YA HEWA
Mwelekeo huu umezingatia hali ya mifumo ya hali ya hewa iliyopo, inayotarajiwa na athari zake kwa msimu ujao wa mvua za Masika (Machi hadi Mei, 2014).

Uchambuzi wa hali ya joto la bahari unaonesha ongezeko la joto katika maeneo ya kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi ambalo linatarajiwa kuendelea kuongezeka kwa kipindi chote cha msimu.  Wakati huo huo, joto la wastani linatarajiwa katika maeneo ya magharibi mwa Bahari ya Hindi na Pasifiki wakati wa msimu. Kwa upande mwingine, joto la chini ya wastani linatarajiwa kuendelea kuwepo kwa kipindi chote cha msimu katika maeneo ya mashariki mwa Bahari ya Atlantiki. Hali ya joto la bahari lililopo na linalotarajiwa kuwepo, linategemewa kusababisha ongezeko la upepo wenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo kuvuma kuelekea katika maeneo ya magharibi na kati ya nchi hususani katika miezi ya Aprili hadi Mei, 2014.

Joto la juu ya wastani iliyopo katika maeneo ya ncha ya kusini mwa bara la Afrika inatarajiwa kuendelea kuwepo katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2014, hali hii inatarajiwa kusababisha mifumo ya migandamizo mikubwa ya hewa iliopo katika maeneo hayo kuwa hafifu. Hali hii inatarajiwa kudhoofisha ukanda wa mvua (ITCZ) katika maeneo ya Pwani ya nchi yetu, hivyo kupelekea kuwepo kwa upungufu wa mvua katika msimu wa masika. Hata hivyo, kuelekea mwishoni mwa msimu, upepo unaovuma kutoka mashariki unatarajiwa kuimarika na hivyo kuwa na uwezekano wa kuwepo kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya Pwani.


D: MWELEKEO WA MVUA: MACHI HADI MEI (MAM), 2014
(i) Mvua za Masika
Maeneo ya kaskazini mwa nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2014. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:
Kanda ya Ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera,Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi katika mikoa ya Kagera na Geita  na kusambaa katika maeneo mengine ya mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu wiki ya pili ya mwezi Machi. Maeneo haya yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani, isipokuwa maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Mara ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi, 2014 na zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani isipokuwa maeneo yaliyopo magharibi mwa mkoa wa Morogoro ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili hadi ya tatu ya mwezi Machi, 2014. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi isipokuwa kwa baadhi ya maeneo yaliyoko mashariki mwa mkoa wa Kilimanjaro ambapo mvua za chini ya wastani zinatarajiwa.
(ii) Mvua za Msimu
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi):
Mvua zinazoendelea katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za wastani kwa ujumla, hata hivyo  mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa mkoa wa Tabora. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2014.

Kanda ya Kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani. Msimu wa mvua unatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2014.
Ukanda wa pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi):
Mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo ya kaskazini mashariki mwa mkoa wa Lindi ambapo mvua za chini ya wastani zinatarajiwa. Msimu wa mvua unatarajiwa kuisha wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2014.
Maeneo ya kusini (mkoa wa Ruvuma):
Mvua zinaendelea katika maeneo haya na zinatarajiwa kuwa za wastani na zinatarajiwa kuisha mwishoni mwa wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2014.
Nyanda za juu Kusini Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Katavi):
Mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo ya mkoa wa Njombe ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha katika wiki ya  kwanza ya mwezi Mei, 2014.

Angalizo: Vipindi vifupi vya mvua kubwa ni matukio ya kawaida hata katika maeneo yanayotarajiwa kuwa na upungufu wa mvua. Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na vimbunga katika bahari ya Hindi na kutoa taarifa kuhusiana na mwelekeo wa mvua nchini pamoja na kutoa tahadhari kila inapobidi.




Kielelezo: Matarajio na mwelekeo wa mvua za Machi hadi Mei 2014
Rangi katika ramani inaonesha matarajio ya mvua kuwa katika madaraja matatu:juu ya Wastani, Wastani na chini ya Wastani. Namba ya juu inaonesha uwezakano wa mvua kuwa juu ya Wastani, ya kati inaonyesha mvua kuwa za Wastani na ya chini inaonyesha  uwezekano wa mvua kuwa za chini ya wastani. Mfano: rangi ya kijani iliyokolea katika maeneo ya Ziwa Victoria na maeneo kusini magharibi ni asilimia 40 juu ya wastani, Wastani ni asilimia  35 na chini ya Wastani ni asilimia 25.

E: ATHARI NA USHAURI
Kilimo na Usalama wa Chakula
Maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na unyevunyevu wa kutosha wa udongo isipokuwa maeneo ya ukanda wa pwani na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba ambayo yanatarajiwa kuwa na upungufu. Katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria (mikoa ya Mara, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Geita na Simiyu pamoja na maeneo ya Morogoro),  wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu za kwaida za shughuli za kilimo. Hata hivyo, mvua za juu ya wastani zinaweza kusababisha unyevunyevu wa kupitiliza unaoweza kuathiri mazao, hivyo wakulima wanashauriwa kufuata ushauri wa wataalam wa kilimo.
                                                                                                            
Katika maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), Wakulima wanashauriwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na kukomaa mapema.

Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Dodoma, Iringa, Lindi, Mtwara pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa Morogoro), hali ya unyevunyevu wa udongo  inatarajiwa kuwa ya kutosheleza, hivyo wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu za kawaida za kilimo. Hata hivyo, mvua za juu ya wastani katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya (Singida, Mbeya, Njombe na maeneo ya Ruvuma) zinaweza kusababisha unyevunyevu wa kupitiliza unaoweza kuathiri mazao na shughuli za uvunaji.

Nishati na Maji
Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani, vina vya maji katika maziwa, mabwawa na mito vinatarajiwa kuongezeka katika kipindi cha msimu wa Machi hadi Mei. Aidha miundombinu ya kuhifadhi maji iboreshwe kwa wakati ili kusaidia uvunaji wa maji katika kipindi cha mvua hizi. Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani, mbinu za kuvuna na kuhifadhi maji zizingatiwe.

Malisho  na Maji kwa ajili ya Mifugo na Wanyamapori
Hali ya malisho na maji  inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi ya nchi isipokuwa maeneo machache ya ukanda wa pwani ambayo yanatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chini ya wastani wafugaji wanashauriwa kuvuna na kuhifadhi malisho kwa matumizi wakati wa kiangazi na  kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa mifugo katika maeneo yao. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani uoto, bioanuai, maua na upatikanaji wa asali na nta vinatarajiwa kuimarika. Aidha, mvua hizo zitasaidia kupunguza  kuhama kwa wanyamapori  na migogoro baina ya wanayamapori na wananchi.
Mamlaka za Miji
Katika kipindi cha msimu wa Machi hadi Mei, vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa  katika baadhi ya maeneo nchini, hivyo mamlaka za miji zinashauriwa kuchukua tahadhari stahiki ikiwa ni pamoja na kusafisha miundo mbinu ya maji taka na mitaro ili kupunguza athari za maji kutuama na mafuriko. Pamoja na matarajio ya mvua za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya ukanda wa pwani na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, kuna uwekano wa kutokea vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo hayo. Hivho tahadhari stahiki zichukuliwe.

Sekta ya Afya
Kwa maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu na chini ya wastani kuna uwezekano wa milipuko ya magonjwa kama vile malaria, kipindupindu, kuhara damu na homa za matumbo. Hivyo, jamii na mamlaka husika zinashauriwa kuchukua tahadhari na maandalizi stahiki ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza. 

Mipango
Sekta mbalimbali za uchumi na kijamii zinashauriwa kutumia taarifa za utabiri wa mvua za msimu wa masika, 2014 katika mipango inayoandaliwa ya utekelezaji na ufanikishaji wa shughuli za taasisi sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Menejimenti za Maafa
Taasisi za maafa na wadau wa sekta husika, wanashauriwa kuchukua hatua muafaka za maandalizi ya kukabiliana na majanga ya hali ya hewa yanayoweza kuathiri jamii na shughuli za kiuchumi.

Mamlaka inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa waendelee kutafuta, kupata  na kufuata ushauri wa wataalamu  katika sekta husika.



Dkt. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI MKUU


No comments:

Post a Comment