Wednesday, February 26, 2014

MJUMBE WA BARAZA LA ARDHI KASAMBYA KIKAANGONI

MJUMBE wa baraza la ardhi la  kata Kasambya katika wilaya ya Misenyi Egidius Medard amehukumiwa na mahakama kwenda jela kutumia kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi 500,000 baada ya mahakama huyo kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zinamkabili.

Hukumu hiyo imetolewa  hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama  ya Bukoba, Sylivia Lushasi jana baada ya mahakama hiyo kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande na mlalamikaji ulioongozwa taasisi ya kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera.

 Tuhuma iliyomtia hatiani Medard ni ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 200,000 toka kwa Haulat Mohamed ambaye alikuwa na mgogoro wa masuala ya ardhi na jirani yake ili ziweze kuwashawishi wajumbe wa baraza la ardhi waweze kutoa hukumu ya upendeleo kwa upande wake.

Mheshimiwa Lushasi alisema mahakama imetoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kata wanaotoa hukumu kwa upendeleo kwa ushawishi wa fedha na mali nyingine.

Amesema vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wajumbe wa mabaraza ya ardhi vya kuomba rushwa ili vipindishe hukumu kuwa kamwe havitavumiliwa, hakimu huyo amesema vinawanyima haki baadhi ya watu wamaostahili kupata zao.

Mheshimiwa Lushasi amemaliza kwa kusema hata vitendo vya watu kujichukulia sheria mikononi vinavyojitokeza ndani ya jamii kwa kiasi fulani vinachangiwa na baadhi ya waliopewa mamlaka ya kusimamia amani ambao wanafanya kazi kinyume na taratibu zinazowaongoza.

Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Fortunatus Mpangamila, awali alisema kuwa Medard alikamatwa na maofisa wa taasisi hiyo julai 5, 2011 akiwa kwenye harakati za kupokea kiasi cha shilingi 200,000, alisema maofisa hao walimnasa Medard baada ya kumuwekea mtego.

Hata hivyo Medard alipelekwa gerezani baada kukosa faini ya shilingi 500, 000 ambayo alipaswa kuitoa kama adhabu hivyo atatumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani.

No comments:

Post a Comment