Wednesday, January 29, 2014

WAZIRI MKUU ATAKA WAKAZI PUGU WAJIUNGE KWENYE SACCOS


*Azindua kisima cha maji, awapigia debe kwenye umeme
*Amtaka RC Dar azuie michango ya darasa la kwanza

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wakazi wa Dunda ‘A’ na Dunda ‘B’ wajiunge kwenye Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na wavisajili kwenye Halmashauri yao ili waweze kukubalika kupatiwa mikopo.

Alikuwa akizungumza na wakazi wa eneo hilo jana jioni (Jumanne, Januari 28, 2014), lililopo Mtaa wa Kigogo Fresh Kata ya Pugu wilaya ya Ilala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kwenye hafla fupi ya uzunduzi wa kisima cha maji kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo.

Waziri Mkuu aliwataka wasajili vyama vyao ili waweze kutambulika kwa urahisi na waweze kuwa na watu wenye dhamana ya kurejesha mikopo mara watakapoanza shughuli za ujasiriamali.

“Tatizo letu ni ukosefu wa anuani za makazi ili wakopaji watambulike na waweze kurejesha mikopo. Tunasisitiza SACCOS kwa sababu tunajua kutakuwa na watu wenye dhamana ya kusimamia urejeshwaji wa mikopo hii,” alisema wakati akijibu swali la Bw. Abdallah Mwaking’inda na wakazi wa Dunda.

Vilevile, alitumia fursa hiyo kumwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadick afuatilie shule ambazo zinatoza michango kwa watoto waliopaswa kuandikishwa darasa la kwanza lakini wakashindwa kuazna shule kwa sababu ya michango hiyo.

“Uandikishwaji wa watoto wanaoanza darasa la kwanza ni wa lazima kwa kila mtoto, tulifanya hivyo ili tuhakikishe watoto wote wapate elimu. Sasa kama mzazi ana watoto wawili au watatu akishindwa kuwalipia manake watoto hao wamebaki nyumbani,” alisema.

“RC litazame vizuri suala hili kwa sababu kama zoezi la uandikishaji ni hili, ina maana kuna wazazi watashindwa kuwapeleka watoto shule,” alisema.

Mapema, kwenye risala yao, wakazi hao wa Dunda ‘B’ walimshukuru Waziri Mkuu kwa kuwaunganisha na mfadhili kutoka taasisi ya REHEMA ambayo imewajengea kisima hicho chenye urefu wa mita 90, tenki la lita 10,000 na mnara wa mita 20 wa kuwekea tenki hilo kwa gharama ya sh. milioni 20.

Walimuomba pia Waziri Mkuu awasaidie kupata umeme wa three phase ili uweze kutosheleza mahitaji ya eneo zima la Dunda ikiwa ni pamoja na kuendesha kisima chao.

Akijibu haoja hiyo, Mhandisi Theodori Bayona kutoka TANESCO makao makuu alisema watarudisha huduma ya three phase iliyokuwepo zamani lakini ikaondolewa kwa sababu ya wizi wa mara kwa mara. Aliwaomba wakazi hao wawe walinzi wa nyaya pindi watakapowekewa na kwamba watatakiwa kulipia service line ya kawaida ili umeme upelekwe hadi kisimani moja kwa moja.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadick aliwahidi kuwachangia tenki moja la lita 10,000 ili waweze kuwa na ujazo mkubwa wa maji kwenye matenki yao na kuepusha kazi ya kupampu maji mara kwa mara.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, wenye magari yanayobeba maji, wanauza ndoo moja kwa sh. 400/- katika eneo hilo.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.

No comments:

Post a Comment