Sunday, November 17, 2013

Rais Kikwete akabidhiwa ripoti kuhusu ugonjwa wa mnyauko wa minazi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali  imedhamiria kukabiliana na maradhi ya mazao likiwamo zao la mnazi ambalo linakabiliwa na tatizo la mnyauko.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu kwa Serikali kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo la minazi kwa sababu watu wengi katika baadhi ya maeneo ambayo uchumi wake unategemea zao la mnazi wanakabiliwa na hatari ya kweli kweli ya kuathirika kwa maisha yao.
Rais Kikwete ametoa uhakikisho huo jana, Jumamosi, Novemba 16, 2013, wakati alipokutana na Waziri wa Maendeleo ya Minazi na Maendeleo ya Shamba la Janatha wa Sri Lanka, Mheshimiwa Jagath Pushpakumara na ujumbe wake mjini Colombo. Waziri huyo aliandamana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti ya Minazi ya Sri Lanka.
Rais Kikwete yuko nchini Sri Lanka kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Madola (CHOGM) unaomalizika leo, Jumapili, Novemba 17, 2013. Mkutano huo wa siku tatu, ulianza juzi, Ijumaa, Novemba 15, 2013.
Mheshimiwa Pushpakumara na ujumbe wake walikuwa wanamwelezea na kumkabidhi Rais Kikwete Ripoti ya Magonjwa ya Minazi iliyoandaliwa na wataalam wa minazi wa Sri Lanka ambao walitembelea Tanzania Julai mwaka huu.
Wataalam hao walitembea Tanzania na kufanya utafiti kuhusu ugonjwa unaolikabili zao la minazi kufuatia ahadi ya Rais Mahinda Rajapaksa aliyoitoa kwa Rais Kikwete wakati alipofanya ziara rasmi ya Tanzania Juni 27, 2013, na baadaye kushiriki katika Mkutano wa Smart Partnership Juni mwaka huu.
Rais Rajapaksa alitoa ahadi hiyo baada ya kuelezwa na Rais Kikwete kuhusu zao la kukauka kwa minazi nchini. Mnazi ni zao muhimu sana katika uchumi wa Sri Lanka na ni zao tegemeo kwa wananchi wa Taifa-Kisiwa hilo kilichoko kusini mashariki mwa India katika Barahri ya Hindi.
Wataalamu waliofuatana na Waziri huyo wamemwambia Rais Kikwete kuwa ugonjwa unaolikabili zao hilo la minazi ambao pia unashambulia minazi katika eneo la Caribbean hauna tiba kwa sababu mpaka sasa hakuna taasisi yoyote ya utafiti imegundua dawa hiyo.
Wataalam hao ambao walikaa Tanzania kwa wiki moja, zikiwamo siku mbili katika Zanzibar, wanasema kuwa zao hilo la mnazi, kama ilivyo katika nchi nyingine zinazolima zao hilo, lina uwezo mkubwa wa kusaidia uchumi kupitia viwanda vidogo vidogo.
Wakati wakiwa Tanzania, wataalam hao wa Sri Lanka walifanya uchunguzi na utafiti kwa karibu na wataalam wa Taasisi ya Utafiti ya Kilimo ya Mikocheni (MARI).
 

No comments:

Post a Comment