Sunday, November 24, 2013

Ngugi wa Thiong'o aheshimiwa Tanzania



Ngugi wa Thiong'o aliyepiga magoti akitunukiwa digrii ya heshima na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania mwishoni mwa wiki kilitunuku digrii ya Heshima Mwana fasihi na mwandishi wa vitabu maarufu Afrika Profesa Ngugi wa Thiong'o.
Ngugi alitunikiwa digrii ya Uzamivu wa Fasihi "Doctor of Literature" ambayo ni ya pili kutunikiwa barani Afrika baada ya aliyotunikiwa kutoka Chuo Kikuu cha Walter Sesulu cha Afrika ya Kusini.
Raia huyo wa Kenya ambaye aliwahi kukimbilia uhamishoni baada ya maandiko yake kupingana na serikali ya Kenya sio mgeni nchini Tanzania kwani baadhi ya vitabu vyake vimeorodheshwa katika mitaala ya shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu nchini humo.
Akizungumzia kuhusu heshima hiyo aliyopewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ngugi amesema amefurahishwa kwa kuwa Chuo hicho kikuu kimetambua mchango wake katika fani ya fasihi na uandishi wa vitabu.
Akizungumzia kuhusu waandishi vijana wanaochipukia Ngugi amesema amefurahishwa kuona na baadhi ya waandishi vijana ambao wanafuata nyayo zao kwa kuandika mambo yanayogusa jamii na kuibua mambo mazito.
Kuhusu maono ya kuandika kitabu kitakachohusu matukio yaliyotokea Kenya hivi karibuni Ngugi amesema anatafakari na upo uwezekano akaandika kitabu kinachohusu hayo yaliyotokea.

No comments:

Post a Comment