Saturday, November 30, 2013

Ndege iliyopotea Msumbiji yapatikana


 
Ndege hiyo ilitakiwa kutua kwenye uwanja wa Luanda.
Ndege iliyopotea tangu jana baada ya kuruka kwenye anga ya Msumbuji kuelekea Angola ikiwa na watu 34 imepatikana katika mbuga za wanyama Kaskazini Magharibi mwa Namibia.
Msemaji wa Polisi nchini Namibia amesema ndege hiyo iliteketea yote huku kukiwa hakuna aliyenusurika.
Ndege hiyo namba TM470 iliondoka Maputo nchini msumbiji tangu siku ya ijumaa na ilikuwa ikielekea Luanda nchini Angola.
mabaki ya ndege hiyo iliyoteketea kabisa yamepatika kwenye mbuga ya wanyama Bwabwata karibu na mpaka wa Angola na Botswana.
"Ndege imeteketea yote yamebaki majivu tu hakuna hata mtu mmoja aliyenusurika," Naibu Kamishna wa Polisi nchini Namibia Willy Bampton amenukuliwa na shirika la habari la Reuters.
Inaelezwa kuwa masiliano ya mwisho na ndege hiyo yalikuwa ni wakati ndege hiiyo ilipofika kaskazini mwa Namibia.
Kwa mujibu wa shirika la ndege la Msumbiji abiria walipanda ndege hiyo ni raia 10 wa Msumbiji, Angola 9, Wareno 5, Mfaransa 1 , Mbrazili 1 na Mchina 1.
Jopo la watu waliokuwa akifanya kazi ya kuitafuta ndege hiyo walishindwa kuingia kwenye mbuga hiyo hapo jana baada ya mvua kubwa kunyesha kufanya barabara kushindwa kupitika.
Abiria 28 na wafanyakazi sita walikuwa kwenye ndege hiyo wakitoka Maputo kuelekea Luanda.

MWENYEKITI WA CHADENA MKOA WA LINDI AUANDIKIA BARUA UONGOZI WA CHADEMA YA KUJIHUDHURU


ALLY OMARY CHITANDA
MWENYEKITI WA CHADEMA
MKOA WA LINDI

30/11/2013

KATIBU WA CHADEMA
MKOA WA LINDI


YAH; KUJIUZURU UENYEKITI WA MKOA

Somo la hapo juu lahusika.

Napenda kuchukua nafasi hii kukuarifu kuwa kwa hiari yangu bila ya kushawishiwa na mtu yeyote, nimeamua kujiuzuru nafasi ya Uenyekiti wa Mkoa tangu leo tarehe 30/11/2013.

Nashukuru sana kwa ushirikiano wako pamoja na Vionmgozi wote wa Baraza la Uongozi pamoja na Baraza la Mashauriano la Mkoa, lakini pia niwashukuru Viongozi wote wa Majimbo naWilaya hasa Nachingwea ambao kwa kiasi kikubwa, wameniwezesha kufika hapa hasa wakati mgumu wa Ujenzi wa Chama  na  kugombea Ubunge 2005 na 2010.Matarajio yangu ya kuweza kukomboa wanyonge kupitia CHADEMA kwa sasa  sioni kama yanaweza kufikika.

Nitabaki kuwa Mwanachama wa kawaida na ninaahidi kuwa Mwanachama  mwaminifu na pale  nitakapohitajika  nikotayari  kusaidiana na Viongozi  kujenga Chama.Nawataki kazi njema na Ujenzi wa Chama.


Ahsante kwa ushirikiano.


………………………………..
A.O. CHITANDA

Thursday, November 28, 2013

ICC yataka Kenyatta kuwepo mahakamani


Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya
Mahakama ya Kimataifa ya kushughulikia kesi za uhalifu wa kivita, ICC imetengua uamuzi wake wa awali uliomruhusu Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi ya uhalifu wa kivita inayomkabili.
Mahakama hiyo sasa imesema kuwa ni lazima Bwana Kenyatta afike binafsi mbele ya mahakama hiyo kusikiliza kesi yake na ushahidi unaotolewa dhidi yake.
Mahakama hiyo imesema kama sheria inavyotaka, Bwana Kenyatta lazima binafsi ahudhurie vikao vya kesi inayomkabili. Imesema maombi yoyote ya baadaye ya kutaka asihudhurie baadhi ya vikao vya kesi hiyo, yatafikiriwa kutokana na msingi wa suala linaloombewa ruhusa hiyo.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi kwamba hukumu iliyotolewa katika rufaa ya tarehe 25 Oktoba 2013 ya Mwendesha mashitaka dhidi ya William Samoei Ruto na Joshua Arap Sang, imetoa taarifa mpya muhimu ambayo inahalalisha kuangaliwa upya kwa suala la kesi hiyo.
Mahakama ya Rufaa ya ICC imehitimisha kuwa Mahakama ina hiyari kwa mujibu wa kifungu namba 63(1), kinachosema kuwa "mtuhumiwa ni lazima awepo mahakamani wakati kesi inayomkabili ikiendeshwa", lakini hiyari hiyo imewekewa kikomo. Mahakama ya Rufaa imetoa uamuzi kwamba mtuhumiwa kutofika mahakamani, inaruhusiwa pale tu panapokuwa na sababu maalum na za kipekee, na lazima sababu hizo ziwe zinakidhi hoja kwa mtuhumiwa kutofika mahakamani hapo.Imeendelea kusema kwamba uamuzi wa kama mtuhumiwa aruhusiwe kutohudhuria sehemu ya vikao vya kesi yake lazima uzingatie hali halisi ya ombi la mtuhumiwa.
Fatou Bensouda,Mwendesha Mashtaka Mkuu ICC
Awali mahakama hiyo ya ICC katika uamuzi wake wa tarehe18 October 2013, ilitoa masharti kwa upande wa utetezi wa Bwana Uhuru Muigai Kenyatta kuwepo mahakamani hapo wakati wa ufunguzi na kufunga kesi inayomkabili badala ya kuwepo wakati wote. Wakati huo angeweza kusikiliza maelezo kutoka pande zote na kusikiliza maoni ya waathirika wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 nchini Kenya. Pia angetakiwa kuwepo siku ya kufunga kesi hiyo kwa kusikiliza hukumu yake.
Kutokana na uamuzi huo wa kumruhusu Bwana Kenyatta kuhudhuria vikao vya ufunguzi na kufunga kesi yake pamoja na vikao vingine ambavyo angeitwa pale mahakama inapoona umuhimu wa yeye kuwepo mahakamani, mwendesha mashitaka alipinga uamuzi huo tarehe 28 Oktoba 2013, kwa kukata rufaa, akitaka kuangaliwa upya kwa uamuzi wa tarehe 18 Oktoba 2013, ambapo mwendesha mashitaka aliomba mahakama kufuta uamuzi wake wa kumruhusu mtuhumiwa kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi yake na badala yake mahakama izingatie sheria kuu chini ya kifungu cha 63(1).
Bwana Kenyatta ameshitakiwa kama mchochezi asiye rasmi, akikabiliwa na mashitaka matano ya uhalifu dhidi ya binadamu, yakiwemo mauaji, kuhamishwa watu kwa nguvu, ubakaji, utesaji na vitendo vingine visivyo vya kibinadamu, vinavyodaiwa kufanyika wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007-2008.
Mashitaka dhidi yake yalithibitishwa tarehe 23 Januari 2012, na kesi hiyo kukabidhiwa Chemba namba V(b) ya mahakama hiyo ya ICC. Kesi yake imepangwa kuanza kusikilizwa katika mahakama hiyo tarehe 5 Februari 2014.

Njia mpya ya Reli Afrika Mashariki


Njia hii ya reli itaunganisha Kenya na kanda nzima ya Afrika Mashariki na eneo la maziwa makuu
Kenya imezindua rasmi ujenzi wa njia ya Reli itakayounganisha kanda ya Afrika Mashariki na eneo la maziwa makuu ujenzi utakaofadhiliwa na serikali ya China.

Reli hiyo itaunganisha Kenya na Sudan Kusini, DR Congo na Burundi.
Sehemu ya kwanza ya njia hiyo ya reli , itaunganisha bandari ya Mombasa na Mji mkuu Nairobi na kupunguza muda wa safari kati ya miji hiyo kutoka masaa 15 hadi masaa manne tu.
Huu bila shaka ndio utakuwa mradi mkubwa Zaidi kuwahi kujengwa tangu nchi hiyo kujipatia uhuru miaka 50 iliyopita.

Mradi huo utagharimu dola bilioni 5.2 kiasi kikubwa cha pesa hizo kikitolewa na Uchina.
Baadhi ya wakenya wanalalamika kuwa tenda hiyo imetolewa kwa kampuni ya kichina kwa njia isiyofaa.

Rais Uhuru Kenyatta katika hafla ya uzinduzi huo amesema kuwa mradi huu ndio utakuwa kumbukumbu kubwa ya utawala wake Kenya.

Mkataba wa ujenzi wa njia hiyo ya reli, ulifikiwa kati ya Rais Kenyatta na mwenzake wa China Xi Jinping mnamo mwezi Agosti mjini Beijing.

Pia kuna matumaini kuwa njia hiyo ya reli itapunguza msongamano mjini Mombasa moja ya bandari yenye shughuli chungu nzima barani Afrika.

Njia ya reli iliyoko sasa, ni ile iliyojengwa enzi za ukoloni.
Baada ya kukamilika kwa sehemu ya kwanza ya reli hiyo mjini Nairobi, mwaka 2017, itaendelezwa hadi Magharibi mwa DRC hususan mjini Kisangani, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

"Tunachokifanya hapa leo, kitaleta mageuzi makubwa sio nchini Kenya tu bali katika kanda nzima ya Afrika Mashariki,’’ alisema Rais Kenyatta akitaja mradi huo kama jambo la kihistoria.
Aliongeza kusema kuwa mradi huu ni moja ya miradi mikubwa katika maono yake ya maendeleo itimiapo mwaka 2030 kuboresha hali ya miundo msingi nchini humo.

Wednesday, November 27, 2013

MAONYESHO YA BIDHAA ZINAZOTENGENEZWA KUTOKANA NA VIAZI LISHE

Bi. Elizabert Kitundu akikagua bidhaa zinazosindikwa kutokana na Viazi lishe.
Baadhi waandishi wa habari, kulia mi MC maarufu katika mkoa wa Kagera Bw. Rutakwa.
Msanii wa kikundi cha Kasimbo toka Ngote wilayani Muleba akifanya vitu vyake.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Misenyi, Bi Elizabert Kitundu, ambaye alikuwa mgeni rasmi, kulia ni mtafiti mwandamizi wa chuo cha utafiti Maruku Innocent Ndyetabula.
Mambo ya ngoma ya Kasimbo.

MAAFISA MIPANGO MIJI MJIREKEBISHE - PINDA
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka maafisa mipango miji nchini kurekebisha utendaji wao wa kazi ili waweze kubadili taswira mbaya iliyojengeka miongoni mwa jamii dhidi yao.

Ametoa kauli hiyo huo leo mchana (Alhamisi, Novemba 27, 2013) wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Wataalam wa Mipangomiji waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji ulioanza leo jijini Dar es Salaam.

“Taswira ya utendaji kazi katika taaluma ya mipangomiji na katika  sekta  ya  ardhi  kwa  ujumla miongoni mwa wananchi na Serikali siyo nzuri sana. Watafiti wanatueleza kuwa kati ya asilimia 60 na 80 ya makazi kwenye miji  yetu hapa nchini yamejengwa kiholela. Na kwa kiwango hicho hicho wakazi wa mijini wako kwenye makazi hayo na wanaishi kiholela,” alisema.

“Wako wanaosema ninyi ndiyo chanzo cha hiyo migogoro, wako wanaosema ninyi kwa rushwa ndiyo wenyewe, mimi sishangai madai haya ila ninawasihi muwe na roho ngumu katika kushinda vishawishi hivi,” alisisitiza.

Aliwataka wajadili masuala yanayohusu migogoro ya ardhi bainaya wafugaji na wakulima, baina ya mipaka ya vijiji, baina ya wilaya, baina ya wanavijiji na hifadhi za Taifa au maeneo ya uchumbaji madini na kujadili njia za kutatua migogoro hiyo ili kuwa na mipamgo endelevu.

Aliwataka waangalie suala la ukuaji wa miji iliyokaribu na Jiji la Dar es Salaam kwa kuangalia dhana ya miji mikubwa kubeba vijiji vinavyoizunguka na hasa kuangalia uwezekano wa kupunguza mlundikano wa watu katika jiji hilo. “Miji ya Kibaha, Mkuranga na Bagamoyo inatumikaje kusaidia kupunguza msongamnano katika jiji la Dar es Salaam,” Waziri Mkuu alihoji

Alisema wataalamu wa mipango miji wanapaswa kuwa na maono makubwa ya baadaye kama kweli wanataka kupunguza majanga katika siku za usoni. “Angalieni utafiti wa gesi unaoendelea pale Mtwara na mjipange, angalieni mpango wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na kuunganisha na reli ya kati, angalieni Lindi na upatikanaji wa Liquified Naturala Gas (LNG), pangeni miji kwa siku za baadaye siyo sasa,” alisisitiza.
Aliwataka wanataaluma hao wasimamie vema taaluma yao kwani katika miaka 37 ijayo, (mwaka 2050) inakadiriwa kwamba nusu ya watu wote watakuwa wakiishi mijini. “Kuweni wakweli, tumieni weledi wenu la sivyo katika miaka 37 ijayo kama wanavyosema watafiti, itakuwa balaa tupu,” alisema.

Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wataalamu hao kutoka mikoa yote hapa nchini, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka alisema maafisa mipango miji wanakabiliwa na changamoto ya kufikiri na kubuni aina ya miji ambayo itakidhi mahitaji ya jamii ya baadaye.

Alisema hata hivyo maafisa hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kushindwa kutoa maamuzi ama ushauri wa kitaalamu kwa kuhofia kuadhibiwa na madiwani.

Mkutano huo wa siku mbili unafanyika katika hoteli ya Blue Pearl, Ubungo na unatarajiwa kufungwa kesho na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, NOVEMBA 27, 2013

Tuesday, November 26, 2013

DAMPO ENEO LA SOKO LA KASHAI KATIKA MANISPAA YA BUKOBA

Wananchi katika katika soko la Kashai wanaomba dampo hili lihamishwe kwa madai ya kuhatarisha afya zao.

Monday, November 25, 2013

Kamanda wa M23 ajisalimisha Uganda


Waasi wa M23 wametimuliwa kutoka katika maeneo waliyokuwa wamekita kambi
Maafisa wa Serikali ya Uganda wanasema kuwa kamanda wa kijeshi wa wapiganaji walioshindwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC, M23, amejisalimisha kwa utawala wa Uganda.
Ripoti kutoka Uganda zinasema kuwa mamia ya wapiganaji wamejisalimisha pamoja na kiongozi wao, Sultani Makenga.
Wapiganaji hao wamejisalimisha katika eneo la hifadhi ya Wanyama ya Pori ya Mgahinga, kwenye mpaka wa Uganda na DRC.
Mnamo Jumanne M23 walisema kuwa wamesitisha maasi yao ya miezi 20 Mashariki mwa Congo, baada ya kutimuliwa katika ngome zao Mashariki mwa Congo na wanajeshi wa Serikali wakishirikiana na askari wa kudumisha amani wa Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo serikali za Uganda na DRC hazijaweza kuthibitsha madai haya.
Mapema wiki hii, M23 ilisema kuwa inamaliza uasi wake wa miezi kumi na tisa masaa chache baada ya majeshi ya serikali kudai ushindi dhidi ya waasi hao.
Ripoti zinasema kuwa Sultani Makenga na waasi wengine 1,700, wamesalimisha silaha zao na wanazuiliwa na jeshi la Uganda katika kambi ya jeshi ya Mgahinga, karibu na mpaka na DRC.
Mapema wiki hii, maafisa wa DRC walisema Makenga alitoroka na kuingia Uganda au Rwanda.
Uganda imekuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya waasi na serikali ya DRC , ingawa hakuna mkataba wa amani umefikiwa.

900 waliuawa katika vita dhidi ya M23


Wanajeshi wa DRC
Jeshi la congo linasema kuwa mapigano na waasi wa M23 yamesababisha vifo vya zaidi ya wapiganaji 900 tangu mwezi Mei.

Msemaji wa jeshi Genarali Jean-lucien Bahuma alisema kuwa takriban wanajeshi 200 na zaidi ya wapiganaji 700 waliuawa katika mapigano katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Wanajeshi watatu wa amani wa UN pia waliuawa kwenye makabiliano hayo.
Pia wapiganaji 72 wa Rwanda na wapiganaji 28 wa Uganda waliuawa.
Mwanzoni mwa mwezi huu, waasi wa M23 walitolewa na jeshi la serikali iliyoungwa mkono na kikosi cha wanajeshi wapatao 5000 wa Umoja wa Mataifa lakini serikali ya Congo na waasi walikosa kuelewana kuhusu mpango wa baadae wa amani.
Waasi wa M23 walisitisha vita na kujisalimisha baada ya jeshi la DRC kwa ushirikiano na wanajeshi wa UN kupigwa vita vikali na kuwaondosha katika maeneo waliyokuwa wameyateka.
Maelfu ya wakaazi wa Mashariki mwa DRC walilazimia kukimbilia nchi jirani ya Uganda kutafuta hifadhi wakati kundi hilo lilipokuwa linaendesha uasi wao na hata kuuteka mji wa Goma kwa muda.
Kudni la M23 lilifanya vitendo vya kikatili dhidi ya watu wa Mashariki mwa DRC ikiwemo ubakaji na kuwatumia watoto kama wapiganaji.

RAIS KIKWETE NA BAADHI YA MARAIS WASTAAFU WA AFRIKA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea mbele jopo la Marais wastaafu wa Afrika kuhusu  linaloongozwa na Rais Mstaafu wa Msumbiji Mhe Joaquim Chissano
anayefuatana na Rais Mstaafu wa Botswana Mhe Festus Mogae leo Novemba 25, 2013 Ikulu jijjini Dar es salaam. Mhe. Chissano, ambaye ni mwenyekiti wa Jopo
hilo pamoja na Mhe Mogae, walifika Ikulu kusikiliza upande wa Tanzania kuhusu mgogoro wa mpaka na nchi ya Malawi, baada ya kufanya hivyo hivi karibuni
huko Blantyre.

PICHA NA IKULU

Sunday, November 24, 2013

TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) YA LEO KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHADEMA
1. Utangulizi Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. 

Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013.
 
 Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. 

Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.
 
Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. 
Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. 
Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
 
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu.
 Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. 

Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
 
i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
 • Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
 • Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
 • Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
 • Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.

ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.
 
iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini.
 Kama nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. 

Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.
 
iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea.
 Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.
 
v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae. 

Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:
 • Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
 • Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.

vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
 • Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
 • Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
 • Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.

3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA. 
Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:
 1. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
 2. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.

4. Hitimisho Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania.
 Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'.

 Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. 

Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
 
Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
 
Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
 
Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.
 
Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia. 
Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.
 
Kabwe Zuberi Zitto, Mb Dar es Salaam. 24 Novemba, 2013

Washambuliaji wa Westgate walivyopenya KenyaWanamgambo wanne wa kundi la Al Shabaab waliohusika na shambulizi la kigaidi dhidi ya jumba la Westgate nchini Kenya , waliingia nchini Kenya kupitia mpakani kutoka Somalia.
Afisaa mmoja mkuu kutoka mojawapo ya nchi za Magharibi ameambia BBC kuwa wanamgambo hao waliingia nchini Kenya kupitia eneo ambalo hutumiwa na watu wengi kuingia Kenya na kisha kukita kambi katika mtaa wa Eastleigh, mjini Nairobi.
Mtaa huo una wahamiaji wengi wa Kisomali baadhi waliokimbia vita kutoka Somalia.
Washambuliaji wanasemekana waliishi Somalia kwa muda ambako walipata mafunzo yao.
Watu 67 waliuawa kwenye shambulizi la kigaidi lililofanywa na kundi la Al Shabaab dhidi ya jumba la maduka la Westgate katika mtaa wa Westlands mnamo mwezi Septemba.
Al Shabaab lilikiri kufanya shambulizi hilo kwa lengo la kulipiza kisasi dhidi ya serikali ya Kenya kwa kutuma majeshi yake nchini Somalia kupambana dhidi ya kundi hilo.
Hadi kufikia sasa raia wanne wa kigeni wamefikishwa mahakamani baada ya kuhusishwa na shambulizi hilo. Wanadaiwa na polisi kuwapa makao washambuliaji hao mjini Eastleigh.
Washukiwa hao, Mohammed Ahmed Abdi, Liban Abdullah, Adan Adan na Hussein Hassan wamekanusha madai ya kuwapa hifadhi magaidi na kuwasaidia kufanikisha mipango yao.
Afisaa huyo hata hivyo amesisitiza kuwa ni watu wanne pekee walioshambulia jengo hilo kama ambavyo serikali ya Kenya imekuwa ikisisitiza.
Wawili kati ya wale waliofanya shambulio hilo, wamejulikana kutokana na nyaraka za mahakani wakisemekana kuwa Hassan Dhuhulow, anayeaminika kuwa raia msomali mzaliwa wa Norway na Mohammed Abdinur Said.
Washambuliaji hao walikuwa na kile maafisa wa usalama wanasema ni msaada mkubwa ndani ya Kenya.
Lakini hakuna ushahidi kuonyesha kuwa mshukiwa mkuu wa ugaidi, Samantha Lewthwaite, mzaliwa wa Uingereza ambaye ni mjane wa mshambuluaji aliyeshambulia kituo cha treni mjini London Uingereza mwaka 2005, alihusika na shambjlizi hilo.
Taarifa hizi zinaweza kusaidia majasusi kujua uraia halisi wa washukiwa wa shambulizi hilo na uhusiano wao na kundi la kigaidi la Al Shabaab.

Ngugi wa Thiong'o aheshimiwa TanzaniaNgugi wa Thiong'o aliyepiga magoti akitunukiwa digrii ya heshima na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania mwishoni mwa wiki kilitunuku digrii ya Heshima Mwana fasihi na mwandishi wa vitabu maarufu Afrika Profesa Ngugi wa Thiong'o.
Ngugi alitunikiwa digrii ya Uzamivu wa Fasihi "Doctor of Literature" ambayo ni ya pili kutunikiwa barani Afrika baada ya aliyotunikiwa kutoka Chuo Kikuu cha Walter Sesulu cha Afrika ya Kusini.
Raia huyo wa Kenya ambaye aliwahi kukimbilia uhamishoni baada ya maandiko yake kupingana na serikali ya Kenya sio mgeni nchini Tanzania kwani baadhi ya vitabu vyake vimeorodheshwa katika mitaala ya shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu nchini humo.
Akizungumzia kuhusu heshima hiyo aliyopewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ngugi amesema amefurahishwa kwa kuwa Chuo hicho kikuu kimetambua mchango wake katika fani ya fasihi na uandishi wa vitabu.
Akizungumzia kuhusu waandishi vijana wanaochipukia Ngugi amesema amefurahishwa kuona na baadhi ya waandishi vijana ambao wanafuata nyayo zao kwa kuandika mambo yanayogusa jamii na kuibua mambo mazito.
Kuhusu maono ya kuandika kitabu kitakachohusu matukio yaliyotokea Kenya hivi karibuni Ngugi amesema anatafakari na upo uwezekano akaandika kitabu kinachohusu hayo yaliyotokea.

KUJIUZULU MAKAMU MWENYEKITI (BARA)


Salaam,

Napenda kuwasilisha kwako taarifa ya kujiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara kuanzia Leo Ijumaa 22 Novemba 2013 kwa kuchoshwa na Unafiki unaoendelea ndani ya Chama. Napenda ifahamike pia kwangu maslahi ya Wapiga kura, Wakaazi na wananchi wa Mpanda Mjini na Wilaya ya Mpanda ni muhimu katika kuwatumikia, hivyo basi sipo tayari kuchaguliwa marafiki.

Kwa kipindi kirefu zimekuwepo shutma dhidi yangu na kutiliwa mashaka mahusiano yangu na Mhe Pinda Waziri Mkuu pamoja na kulijadili katika vikao kadha Mpanda na Dar es Salaam bado yapo mashaka kwa nini alipita bila kupingwa hayo yalikua maamuzi ya Wanampanda kwenu imekua ni tatizo lakin hamsemi kwa nini Majimbo mengine 16 nchini yalipita bila kupingwa mlikua wapi na nani alaaumiwe huu ni Unafiki  wa kupindukia.

Aidha mmechukizwa sana kwa nini nilihoji kauli ya Muasisi wa Chama Mhe Mtei kutuchagulia viongozi naomba ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo wangu na utabakia hivyo siku zote kwa chama cha demokrasia kutoruhusu uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya Waasisi ambao huvigeuza vyama kuwa Mali binafsi

Kwa kusema ukweli na kusimamia ukweli daima itabakia kuwa lengo langu katika maisha yangu siku zote hata kama itanigharimu maisha yangu

Nawasilisha.


Said A Arfi (mb)

Thursday, November 21, 2013

MSIMU WA SENENE WAANZA RASMI MKOANI KAGERA


Senene hao.
Senene wakiwa wamepakiwa kwenye vyandarua vinavyotolewa na serikali kwa ajili ya kuzuia mbu waenezao malaria.

Wednesday, November 20, 2013

PRESIDENT JAKAYA KIKWETE IN POLAND

  President Jakaya Mrisho Kikwete with Minister of State in the Vice President's Office Dr Theresia Huvisa and Minister of State in the Zanzibar Second Vice President's Office Hon. Fatma Fereji after addressing  a High-level meeting on 'Caring for Climate' business Dialogue alongside the on-going UN Climate Change Conference (COP19/CMP9) in Warsaw, Poland. 

President Jakaya Mrisho Kikwete addresses a High-level meeting on 'Caring for Climate' business Dialogue alongside the on-going UN Climate Change Conference (COP19/CMP9) in Warsaw, Poland. With him are UN Secretary General Ban Ki Moon, COP19/CMP9 President Marcin Korolec and other dignitaries.

PINDA AFUNGA MAONYESHO YA BIASHARA AFRIKA.

  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akipata maelezo kutoka kwa Bw. Gerge Buchafu wa Shirika la  Maendeleo ya Viwanda Vidogovidogo (SIDO)  baada ya kufunga  maadhimisho ya siku ya viwanda  Afrika  kwenye  uwanja  wa Maonyesho wa Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam,  Novemba 20, 2013. Kulia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dr. Abdallah Kigoda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Waziri wa Viwanda na Biashara , Dr Abdallah Kigoda wakati alipofunga  maadhimisho ya siku ya  Viwanda Afrika kwenye uwanja wa maonyesho wa Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam, Novemba 20, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akipata maelezo kuhusu  viatu  kutoka kwa Elizabeth George (kulia)wakati alipotembelea  banda la Woiso Original Products katika maonyesho yaliyoambatana na maadhimisho a siku ya Viwanda Afrika yaliyofaungwa na Waziri Mkuu Novemba 20, 2013 kwenye  uwanja wa maonyesho ya biashara ya kimataifa ya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam . Kushoto kwake ni Waziri wa Viwanda na Biashar, Dr. Abdallah Kigoda na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Tuesday, November 19, 2013

RAIS KIKWETE AWASILI NCHINI POLAND

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili jijini Warsaw, Poland, kuhudhuria mkutano wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Kyoto kuhusu mabadiliko ya Tabia Nchi.


MWENYEKITI WA WA WABUNGE WANAWAKE WA BUNGE LA AFRIKA AWASILI MKOANI KAGERA

Mwenyekiti wa wabunge wa bunge la wanawake la afrika Bi Bernadetha Mshashu muda mfupi baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba.
Bi. Mshashu akisaini kitabu cha wageni.
Akisalimiana na viongozi na wanawake waliofika kwenye uwanja wa ndege kumlaki.
Baadhi ya wanawake waliofika uwanjani kumlaki.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bi Ziporah Pangani kulia alikuwa miongoni mwa wanawake waliojitokeza kumlaki Bi. Mshashu ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu mkoani kagera.
Mstahiki Meya wa manispaa ya Bukoba Anatory Amani mwenye miwami alikuwa miongoni mwa waliojitokeza kumlaki.