Saturday, October 26, 2013

Serikali Kikwazo-Zitto Kabwe



Wakati shinikizo la Dunia sasa limeelekea kumaliza tatizo la ukwepaji kodi na Utoroshaji wa fedha kutoka nchi za Kiafrika, serikali ya Tanzania inavuta miguu.

Moja ya njia ya Serikali za nchi maskini kupata taarifa za makampuni makubwa ya kimataifa(MNCs) yanayokwepa kodi ni mfumo wa kupashana taarifa (automatic exchange of tax information) .

Kufutia shinikizo la nchi mbalimbali, hivi sasa nchi zinazoitwa "secrecy jurisdictions" (tax havens) Zimeanza kuweka sahihi makubaliano ya kutoa taarifa. Tanzania mpaka sasa haijaweka sahihi na serikali haijatoa taarifa yeyote kwa Umma.
Ghana, Afrika Kusini na Nigeria nchi zinazotegemea sana rasilimali kama Tanzania zimeweka saini mkataba huu tayari. Asilimia 44 ya fedha za kigeni nchini zinatokana na mauzo ya madini nje. Makampuni ya madini ndio yanaongoza kukwepa kodi.

Tanzania inapoteza jumla ya dola za kimarekani kati ya milioni 500 na bilioni 1.25 kwa mwaka kutokana na Makampuni makubwa ya kimataifa kukwepa kodi. Hii ni sawa na kusema Tanzania inapoteza dola takribani milioni mbili kila siku kwa uporaji huu.

Naitaka serikali kutoa taarifa kwa nini haichuki hatua kuzuia mwanya huu wa mapato ya Umma. Serikali ichukue hatua mara moja kuhakikisha Tanzania inaingia makubaliano ya kupashana taarifa za kikodi. Huu sio wakati wa kuvuta miguu katika suala nyeti la umma. Badala ya kukimbilia kutoza kodi wanyonge, tuhakikishe makampuni makubwa yanayonyonya rasilimali zetu yanalipa kodi inayotakiwa.

Zitto Kabwe, MB
Waziri Kivuli wa Fedha

24 Oktoba, 2013
Geneva, Switzerland

No comments:

Post a Comment