Monday, October 21, 2013

PROFESA TIBAIJUKA ZIARANI MULEBA KATIKA JIMBO LAKE LA KUSINI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kusini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa CCM yuko katika ziara ya kiaina jimboni kwake. Akidai kwamba hataki kuwasumbua wananchi kwa matayarisho ya ujio wake, anaingia katika kijiji kimoja baada ya kingine na kukutana na wananchi kwa matembezi ndani ya kijiji ili ajithibitishie kwa macho kero na changamoto hizo na kuzitafutia ufumbuzi.

Jumapili tarehe 19 oktoba ametembelea kijiji cha Bihanga kata ya Burungura na kushuhudia shule ya msingi yenye madarasa manne yaliyoezekwa kwa nyasi. Wanafunzi walimueleza adha kubwa wanayoipata wakati wa mvua. Utoro katika shule hiyo ni mkubwa kwa sababu ya mazingira mabaya. Akakaa na viongozi wa kijiji na wananchi na kuamua  kuweka nguvu pamoja kujenga madarasa 4 kabla ya mwisho wa mwaka. Amesema atarejea kwenye uzinduzi wa madarasa hayo mwezi Januari.

Katika kijiji cha Kiga kata ya Rulanda Profesa Tibaijuka alipokelewa na Mwenyekiti wa Kijiji Ndugu Masud Ibrahim. Aliandamana na wanawake vijana na watoto ambao katika mda mfupi walijitokeza kwa wingi kumlaki mara baada ya kusikia ujio wake,  kuteka maji katika chemchem pekee ya Nyakashengya inayotegemewa na kijiji hicho. Profesa aliteka dumu la maji kwa bibi kizee mmoja mama Mwajabu ambaye hajiwezi tena.


Kwa mila na desturi mwanamke huwezi kwenda mtoni ukarejea nyumbani bila maji kuwasaidia wasiojiweza! Hiyo ni kupoteza wakati? Profesa Anna alishuhudia uharibifu mkubwa wa chanzo hicho na ufugaji holela wa mifugo inayotoka vijiji jirani ikiwa mali ya wafugaji wakubwa.

 Aidha Mwenyekiti na wanawake walimuonyesha kwa uchungu mashamba yao ya mihogo yaliyoharibiwa kabisa na makundi ya ng'ombe hao. Kijiji hicho zamani kilikuwa kinazalisha mihogo kwa biashara lakini sasa hawana hata ya kula wao wenyewe kwa sababu ya uharibifu wa mifugo.

 Profesa Tibaijuka aliahidi kuleta mainjinia kuboresha chanzo cha maji na kutenga sehemu ya kuteka maji, kunywesha mifugo na kufua nguo. Kwa kuwa tayari kijiji kina mpango wa matumizi bora ya ardhi alitoa Shs laki tano kwa vijana kuunda kikosi cha ulinzi wa mashamba. Wanawake walidai wanaogopa kwenda kulima kwa sababu wanafukuzwa na kupigwa na wachungaji hao.

 Waziri Tibaijuka aliagiza kuwa mifugo yote itakayokutwa katika mashamba ikamatwe na kupelekwa kwa Mkuu wa Wilaya kwa sababu wananchi walidai hawana imani na polisi.

Akipita ndani ya kijiji alitembelea yatima 2  waliomaliza darasa la saba na kujitolea kuwalipia karo wakifaulu kwenda sekondari. Aidha alitoa mchango wa kujenga darasa moja la sekondari ya Rulanda, kuezeka madarasa mawili shule ya msingi ya kijiji jirani cha Nyabule ambayo imekwama mda mrefu.


 Alitoa mchango wa laki mbili na nusu kwa vikundi 4 vya wanawake ili waboreshe mtaji wao. Katika mkutano wa hadhara uliotawaliwa na ngoma hoihoi na vifijo kumpokea mbunge wao, Profesa Anna aliwaasa vijana kuwa na nidhamu na kutodanganywa na wapiga porojo na kejeli  bila matendo yoyote. 

Alisema vijana watambue kuwa tofauti za itikadi hazitakiwi kuleta uhasama na vurugu. Akawaeleza kuwa watambue kuwa nguvu na jeuri ya ngumi inatokana na utofauti wa vidole! Je kama vyote vingelikuwa saizi moja ngumi ingekuwa na nguvu gani? Kwa mantiki hiyo kila mmoja wetu ana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo awe mke awe mume, awe CCM au Chadema au CUF.

 Cha msingi ni kauli na hoja zake. Aliwaambia vijana wapime akili ya mtu kwa kauli na kazi zake. Mtu asiye na heshima hawezi kuleta maendeleo yoyote. Na Kiongozi anayesubiri utawala kwanza ndiyo ashughulikie matatizo ya wananchi ana faida gani?

 Alisema vijana wasiyumbishwe wachambue mambo na waone nani wa kuwaongoza.  CCM ina mengi ya kurekebisha lakini pia imefanya mengi. Umati ulimshangaa kwa busara na uelewa wake wa mambo na kumsikiliza kwa makini. Kero ya wanyama waharibifu wa mazao nyani tumbili na viboko alisema atazitafutia ufumbuzi haraka iwezekanavyo. Sherehe ilimalizika kwa chakula cha pamoja.

Awali Katika kata ya Gwanseli  Profesa Tibaijuka alisali misa ya jumapili katika Kanisa la Kilutheri KKKT la ilemera ambapo Alitembelea shule ya ufundi yenye uwezo wa kuwafundisha wanafunzi 22 kwa mwaka vijana 10 wanajifunza useremala na wasichana 12 ushonaji na elimu ya nyumbani. Wote ni yatima na wanafadhiliwa na Swedeni. Profesa Tibaijuka alichanga lhaki mbili na nusu kuwasaidia. Aidha alitembelea dispensari ya Ilemera na kushuhudia wagonjwa kupungua baada ya mlipuko wa malaria wilayani muleba kuthibitiwa.

No comments:

Post a Comment