Sunday, September 08, 2013

SERIKALI KUTOVIOKOA VYAMA VYA USHIRIKA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa siyo kazi ya Serikali kuviokoa vyama vya ushirika kutoka kwenye madeni kwa sababu shughuli za ushirika ni za sekta binafsi na mali ya wanachama wenyewe.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa makosa ya ushirika na wezi wa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika hatimaye yanabebeshwa vyama vya siasa.
Kama namna ya kuwasaidia wananchi, Rais Kikwete amewataka viongozi mbali mbali wa mikoa kuwasaidia wananchi ili kupata viongozi waadilifu na waaminifu na wala siyo wezi kama ilivyo sasa kwa vyama vingi vya ushirika.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo, Jumamosi, Septemba 7, 2013, wakati alipopokea Ripoti ya Maendeleo ya Mkoa wa Mwanza kwenye Ikulu Ndogo mjini Mwanza kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo.
Rais Kikwete aliwaambia viongozi hao wa Mkoa wa Mwanza: “Tumewahi huko nyuma kulipa madeni yote ya vyama vya ushirika. Nia ilikuwa kuvisaidia vyama hivyo na wanachama wake kujipanga upya na kupata uhalali wa kuweza kukopa fedha za kjuendesha shughuli zao. Lakini sasa, vyama hivyo, vimerudi kule kule kwenye madeni.”
Alitoa mfano wa Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Pwani kama moja ya vyama vya ushirika ambavyo madeni yake yalilipwa na Serikali lakini sasa kina deni kubwa zaidi kuliko hata lile lililolipwa na Serikali.
“Wale watu wa Pwani walikwenda kukopa na benki moja ikakubali kuwapa fedha. Wameshindwa kulipa na ule ushirika nadhani utakufa. Njia bora kwa vyama vya namna hiyo ni kuviachia vife tu kwa sababu havina faida yoyote kwa mkulima.”
Aliongeza: “Vyama vya ushirika siyo mali ya Serikali. Ni mali ya wanaushirika na hivyo ushirika ni sekta binafsi. Lakini hakuna shaka kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wanatesa wananchi. Wanakopa fedha kwenye mabenki lakini wanashindwa kuzirudisha fedha hizo na hilo linapotokea Serikali inalaumiwa kwa hali hiyo.”
Rais alikuwa anatoa maelekezo yake baada ya kuambiwa kuwa Chama cha Ushirika cha Nyanza cha Mkoa wa Mwanza kilikuwa kinakamilisha mpango wa kukopa kiasi cha sh bilioni saba kutoka Benki ya Raslimali Tanzania (TIB) kwa ajili ya kununulia pamba.
Lakini aliwaambia viongozi hao: “Uamuzi wa kukopa ama kutokukopa ni wa kwenu. Nyanza ni mali yenu, wezi waliopata kukibebesha madeni chama hicho mliwachagua nyie wenyewe. Fedha ni zenu lakini hatimaye athari za makosa yenu yanaiathiri Serikali na hata vyama vya siasa.”
“Kuna wakati viongozi wa Chama cha Nyanza walipata kuuza godown ya thamani y ash milioni 600 kwa sh milioni 50 tu. Hawa ni wezi wa mchana wanaoiba kweupe. Wanaiba lakini wanataka Serikali iwasaidie. Kwa nini? Nadhani kazi yetu kama viongozi ni kuwasaidia wananchi kupata viongozi adilifu na aminifu siyo wezi,” alisema Mheshimiwa Rais Kikwete na kuongeza:
“Tatizo ni kwamba hata sisi viongozi tunakataa kuwashughulikia wezi kwa sababu hawa ni watu maarufu na wakati mwingine baadhi ya viongozi wanakula nao na jambo hilo limekuwa tatizo kubwa sana. Tunavifikisha vyama vya ushirika mahali ambako sina uhakika kama bado ni mali ya wakulima. Wakulima wanakutana na ushirika wakati wa kuchagua viongozi tu na baada ya hapo wakulima hawaonekani tena.”
           

No comments:

Post a Comment