Tuesday, September 03, 2013

ICC - Bunge la Kenya kujadili kujiondoa



Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto
Bunge la Kenya limeitisha kikao cha dharura kujadili kujiondoa kwa nchi hiyo kama mwanachama wa Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu ICC.
Naibu wa Rais wa Kenya William Ruto alikuwa amepangiwa kufika mbele ya mahakama hiyo ya ICC wiki ijayo kujibu mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu. Naye rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kufika mbele ya mahakama hiyo mwezi Novemba.
Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na shinikizo kutoka kwa wabunge na wanachama wa chama kinachotawala cha Jubilee kutaka kuondolewa mashtaka yanayowakabili viongozi Uhuru Kenyatta na William Ruto.
Naibu wa Spika Joyce Laboso amepanga kikao hicho kufanyika Siku ya Alhamisi. Hata hivyo hata ikiwa bunge hilo litapitisha hoja hiyo, kujiondoa kama mwanachama wa ICC, ni uamuzi ambao lazima ufikishwe kwa wananchi katika kura ya maoni.
Baada ya kupita hapo ndipo itawasilishwa kwa baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kupata idhini na kueleza sababu kamili za kutaka kuchukua hatua hiyo, pamoja na kuwa wananchi wenyewe wameamua.
Hata hivyo kwa mujibu wa sheria za mahakama hiyo ya ICC, hata kama nchi itajiondoa kama mwanachama, kesi ambazo zilikuwa tayari zimeshawasilishwa katika mahakama hiyo kuwahusu raia wa nchi hiyo, lazima zitaendelea kusikizwa hadi mwisho na hukumu kutolewa.
Kwa hiyo hata ikiwa Kenya itajiondoa sasa, viongozi wao Uhuru Kenyatta na William Ruto bado wanayo mashtaka ya kujibu mbele ya mahakama ya ICC.

No comments:

Post a Comment