Wednesday, August 28, 2013

Urusi yapinga azimio la kuiadhibu Syria


Rais wa Marekani Barack Obama
Marekani imeachana na jitihada za kutafuta uungwaji mkono wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuichukulia hatua Syria kwa utumiaji silaha za kemikali.
Hii ni kufuatia kukataa Urusi kwa rasimu ya maazimio yaliowasilishwa kwenye mkutano wa wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo la usalama.
Akilaumu Urusi kwa kile alisema msimamo wake wa kutobadili maoni kwa chochote, Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni, Maria Harf amsema kuwa Marekani haitaruhusu alichotaja kama uzembe wa kidiplomasia kutumiwa kama ngao ya kutetea Serikali ya Syria. Azimio lilioandikwa na Uingereza lingaliruhusu hatua za kuwalinda raia wa Syria lakini likapingwa na Urusi katika kikao cha wanachama watano wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wataalamu wa Umoja wa mataifa wa silaha za kemikali
Urusi, ambayo hutoa silaha kwa Serikali ya Syria na pia mshirika wake mkuu kimataifa, ilisema kuwa kura ya azimio hilo inapaswa kuahirishwa hadi tume maalumu ya umoja wa mataifa ya kuchunguza matumizi ya silaha za kemikali nchini humo itakapokamilisha kazi yake.
Msemaji huyo alielezea hali ya Marekani ya kutoridhika na hali ya upole inayoendelea katika Umoja wa Mataifa, na akasisitiza kwamba kwa wakati huu Marekani haioni matumaini yoyote ya kuungwa mkono na Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa na kwa sasa itatilia mkazo mashauriano na mataifa mengine washirika kabla ya kuchukua hatua yoyote inayofaa hivi karibuni.
Alisema kuwa hadi kufikia sasa Rais Obama hajafanya uamuzi wowote juu ya hatua inayopaswa kuchukuliwa, lakini akaongeza kuwa ni dhahiri kuwa silaha za kemikali zilitumiwa nchini Syria na kwamba wa kulaumiwa ni utawala wa Rais Assad.

No comments:

Post a Comment