Wednesday, August 21, 2013

HATI ZA KUMILIKI ARDHI ZITOLEWE UPYA, ZA DIJITALI NA ZIHUSISHWE NA NAMBA YA MLIPA KODI (TIN)
 
Kamati ya Hesabu za Serikali imekutana na Wizara ya Ardhi kwa madhumuni ya kupitia Hesabu za Wizara kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2012. Changamoto za Wizara ni nyingi sana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amehoji mambo mengi sana na mengi ni wizi, upotevu wa mapato ya Serikali na malalamiko ya wananchi kuhusu ardhi.  CAG alitoa hoja za ukaguzi maeneo ya mapato kutokusanywa, kulimbikizwa na hata kukusanywa bila kuyawasilisha Wizarani.
 
Katika Mwaka wa Fedha 2011/12 Wizara ilipangiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni tisini na tisa (99 bilioni) lakini ilikusanya shilingi bilioni ishirini tu (20 bilioni) sawa na asilimia 21 ya makadirio.
 
CAG pia alihoji masuala ya viwanja vilivyopimwa, kugawiwa watu lakini watu hawakupewa hati ambapo zaidi ya viwanja 7, 342 vilikutwa ni viwanja vyenye shaka. Pia viwanja 160 jijini Dar es Salaam vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 555.8 milioni viligundulika ni viwanja ambavyo walijigawiwa maafisa wa Ardhi maana haoakuwa na ushahidi wowote wa mauzo ya viwanja hivyo. Hoja nyingine ni pamoja na ukiukaji wa sheria kwa kujengwa kwenye fukwe nk.
 
Katika Ripoti ya Hesabu za Serikali Kuu 2011/12 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alipendekeza kuanzishwa kwa haraka mfumo fungamanifu wa Taarifa za Ardhi, kutunza kumbukumbu kielektroniki na kuunganisha kuanzisha utaratibu wa kwamba wakati wa kusajili hati ya ardhi anayesajili kuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN).
 
Baada ya mjadala wa kina na kushauriana na wakaguzi na wataalamu Kamati ya Hesabu za Serikali iliona kuwa kuna haja kubwa sana ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye mfumo mzima wa kutoa hati za kumiliki Ardhi. Hivyo Uamuzi mkubwa tuliochukua ni kuagiza kuwa hati zote za kumiliki ardhi zitolewe upya, ziwe za dijitali na hati ziendane na namba ya Mlipa kodi (TIN). 
 
Kamati imeagiza kuwa  Wizara kutoa majibu ya utekelezaji wa agizo hilo ifikapo Mwezi Januari mwaka 2014. Tunaamini kuwa iwapo hati zote za ardhi zitakuwa za dijitali, tutaondoa kabisa tatizo la hati mbili kwenye kiwanja au shamba moja, itakuwa ni rahisi kwa usimamizi wa ardhi na itaondoa mgogoro mingi ya ardhi hapa nchini. Pia tunadhani pia itakuwa rahisi kujua nani anamiliki ardhi kiasi gani, wapi nk. 
 
Tunaamini kuwa mfumo wa dijitali katika hati za ardhi utaongeza usalama zaidi kwa wamiliki wadogo wa ardhi na kuondokana kabisa au kwa kiasi kikubwa na hati za bandia ambazo zinaumiza zaidi wananchi masikini wanaotapeliwa kila wakati. Ardhi yenye hati za kidijitali na zinazotunzwa kielektroniki zitakuwa na thamani zaidi na zitawezesha mahitaji zaidi ya hati hizo kwa shughuli mbalimbali za wananchi.
 
Mapato yatokanayo na umiliki yatakusanywa kirahisi sana na kwa kuwa kila hati itakuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN)  itakuwa ni njia rahisi ya kuzuia ukwepaji kodi ya ardhi.  Kwa kuwa kamati imeagiza kuanza kutumika kwa risiti za elektroniki kwa malipo ya serikali, tutaweza kupandisha mapato ya Serikali na hasa kwenye halmashauri za wilaya na kuepukana na kodi sumbufu kwa wananchi.
 
Changamoto kubwa ni kama matajiri wenye ardhi kubwa watakubali mageuzi haya kwani hawapendi ijulikane kiwango cha ardhi wanachomiliki na pia itazuia ukwepaji kodi na kupunguza rushwa kwa watendaji wa Wizara ya Ardhi. 
 
Mfumo huu hata hivyo uwezeshe watu kuweza kutafuta kwenye mtandao hati, iwe rahisi kutafanya utafutaji. Pia mfumo huu unaweza kusaidia sana suala la fidia kwa wananchi wanaohamishwa kupisha uwekezaji mkubwa kama kwenye sekta za madini na gesi asilia. Kwa mfano mwekezaji atapaswa kuhakikisha hati za kijiditali zinapatikana kwa wananchi wanaohamishwa kupisha mradi baada ya maridhiano ya wananchi hao kuhusu kupisha mradi na mahala watakapohamia.
Kuna haja pia hata hati za madini (mining rights) na leseni mbalimbali ziwe za dijitali na kuhusishwa na TIN. Huko ndipo tunapaswa kuelekea.
 
Zitto Kabwe
MwenyeKiti PAC  
Agosti 21, 2013 - Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment