Tuesday, July 30, 2013

KIKWETE AUPA WAKATI MGUMU UONGOZI WA MANISPAA YA BUKOBA


RAIS wa jamhuri ya muungano wa Tanzania,  Dkt.Jakaya Kikwete ameuagiza uongozi wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba kuhakikisha unagawa viwanja kwa wananchi zaidi ya 800  waliokuwa wanadai viwanja walivyoviomba katika manispaa hiyo mwaka 2003.
 
Rais Kikwete alitoa agizo hilo wakati akiwahutubia wananchi wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba katika  mkutano wa hadhara kwenyeuwanja wa michezo wa Kaitaba baada ya kupokea taarifa toka mbunge wa jimbo la Bukoba mjini Balozi Khamis Kagasheki juu ya malalamiko ya wananchi walioomba viwanja katika manispaa hiyo.
 
Aliuambia uongozi huo pia kuhakikisha unawarejeshea wananchi hao fedha walizozitoa wakati wa mchakato wa kuomba viwanja hivyo, ameutaka uongozi huo kutekeleza haraka mchakato wa kuwapatia viwanja hivyo kwa wananchi hao.

Aliuambia uongozi huo utenge viwanja 800 kutoka  kwenye viwanja vya mradi vya upimaji wa viwanja 5,000 ambavyo halmashauri ya manispaa ya Bukoba imeanza kuviuza kwa wananchi.

 
Alisema atauelewa uongozi wa manispaa hiyo ikiwa utashidwa kutekeleza agizo alilolitoa, “lazima haki ya wananchi itendeke, haki itatendekeka ikiwa manispaa itawapatia wananchi viwanja walivyoviomba ambavyo hawajapatiwa kwa muda mrefu” aliagiza.
 
Pia katika mkutano huo aliwaeleza wananchi  mradi  wa ujenzi wa soko kuu la Bukoba  kuwa lazima utekelezwe, Rais huyo aliuagiza uongozi manispaa kuhakikisha unaandaa maeneo mbadala yatakayotumiwa na wafanyabiashara watakaohamishwa katika soko hilo la sasa baada ya kuvunjwa kupisha ujenzi wa soko jipya.
Rais huyo alitoa angalizo kwa  uongozi wa manispaa kuhakikisha unatekeleza ujenzi wa soko jipya kwa kufuata taratibu zote zinazokubalika, aliauagiza pia kuwashirikisha wananchi katika mchakato mzima wa ujenzi wa soko hilo jipya.
 
Alisema mradi wa ujenzi wa soko jipya la kisasa unaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo katika manispaa ya Bukoba, “wananchi wanapenda maendeleo ni lazima wakubali mradi wa ujenzi wa soko jipya la Bukoba” alisisitiza.
 
Rais Kikwete aliwaambia wananchi waachane na malumbano ya kisiasa kwa kuwa yanakwamisha mambo ya maendeleo, alisema kuwa maendeleo hayaji mara moja yanataka mchakato, alimaliza kwa kuiwaomba wananchi kuwa kitu kimoja hasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo inayobuniwa.

Kwa sasa uongozi wa manispaa hiyo unatekeleza mradi wa upimaji na wa viwanja 5,000 ambavyo tayari imeishaanza kuviuza kwa wananchi, pamoja na mradi wa upimaji na ugawaji wa viwanja wale walioomba viwanja mwaka 2013 uongozi wa manispaa umewaweka pembeni.
 

No comments:

Post a Comment