Friday, March 29, 2013

JENGO LA GHOROFA 16 LADODOKA RAIS KIKWETE AKAGUA TUKIO

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo toka kwa Mkuu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam Bw. Suleiman Kova na Mkuu wa Mkoa huo Mhe saidi Meck Sadiki katika eneo la  jengo lililoporomoka mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es salaam  asubuhi saa mbili na nusu leo Machi 29, 2013 ambapo hadi Rais anafika mahali hapo saa saba kamili watu wawili wamethibitishwa kuwa wamekufa na wengine 19 kujeruhiwa, wawili wakiwa mahututi. Juhudi zinaendelea kuokoa watu wanaosadikiwa kunaswa kwenye kifusi cha jengo hilo lililokuwa limefikia ghorofa ya 15, likijengwa ubavuni mwa Msikiti wa Shia Ithnaasheri.

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa  mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es salaam leo akiwa ameongozana na mkewe Mama Salma Kikwete kujionea mwenyewe jengo lililoporomoka asubuhi saa mbili na nusu leo Machi 29, 2013 ambapo hadi Rais anafika mahali hapo saa saba kamili watu wawili wamethibitishwa kuwa wamekufa na wengine 19 kujeruhiwa, wawili wakiwa mahututi. Juhudi zinaendelea kuokoa watu wanaosadikiwa kunaswa kwenye kifusi cha jengo hilo lililokuwa limefikia ghorofa ya 15, likijengwa ubavuni mwa Msikiti wa Shia Ithnaasheri.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es salaam leo akiwa ameongozana na mkewe Mama Salma Kikwete kujionea mwenyewe jengo lililoporomoka asubuhi saa mbili na nusu leo Machi 29, 2013 ambapo hadi Rais anafika mahali hapo saa saba kamili watu wawili wamethibitishwa kuwa wamekufa na wengine 19 kujeruhiwa, wawili wakiwa mahututi. Juhudi zinaendelea kuokoa watu wanaosadikiwa kunaswa kwenye kifusi cha jengo hilo lililokuwa limefikia ghorofa ya 15, likijengwa ubavuni mwa Msikiti wa Shia Ithnaasheri.

Thursday, March 28, 2013

SIRI YA KUUWAWA ZITTO

Katika gazeti la Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna habari yenye kichwa chenye maneno ‘ SIRI YA KUUWAWA ZITTO YAFICHUKA’ na vichwa vidogo ‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ dk. Slaa atajwa kumtuma Saanane kummaliza’. Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa. Napenda kusema yafuatayo:
Moja, sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi. Haijawahi kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika na hivyo naomba mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari vimempa habari sahihi.
Pili, Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu. Ndio maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuwawa nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio furaha ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili lakini mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni kufanya kazi zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia ukweli bila kujali uchungu wa ukweli huo.
Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi.
Nne, Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe mfano bora wa kuheshimu demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi kutoa dola kwa chama chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya watu wachache. Tusimamie misingi ya kuanzishwa chama chetu.
--
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar-es-Salaam
Jumatano, Machi 27, 2013
 

SIMBA YASHINDWA KUTAMBA BUKOBA YAFUNGWA 1-0

 Baadhi ya washabiki wakishuhudia mpambano wa soka kati ya timu ya simba na kagera sugar uliofanyika kwenye uwanja wa Kaitaba, katika mchezo huo timu ya kagera sugar iliifunga simba goli 1-0.
 Benchi la timu ya kagera sugar.

 Kocha wa timu ya simba akihaha baada ya timu hiyo kubanjuliwa goli moja na timu ya Kagera sugar kwenye uwanja wa Kaitaba.
 Baadhi ya washabiki wa soka mkoani Kagera.
Benchi la wachezaji wa Timu ya Simba.

RAIS KIKWETE AZINDUA RASMI TAARIFA YA VIASHIRIA VYA UKIMWI NA MALARIA


Meza kuu ikimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiri Ukimwi (TACAIDS) Mama Fatma Mrisho akisoma taarifa ya utafiti wa viashiria vya ukimwei na malaria mwaka 2012 leo Machi 27, 2013 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam.
PICHA NA IKULU

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akinyanyua juu baada ya  taarifa ya utafiti wa viashiria vya ukimwei na malaria mwaka 2012 leo Machi 27, 2013 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam.
Kulia kwake ni Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda',  Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiri Ukimwi (TACAIDS) Mama Fatma Mrisho.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikata ukanda kuzindua rasmi taarifa ya utafiti wa viashiria vya ukimwi na malaria mwaka 2012 leo Machi 27, 2013 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam,Kulia kwake ni Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Saidi Meck Sadiki. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiri Ukimwi (TACAIDS) Mama Fatma Mrisho na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mhe William Lukuvi

Wednesday, March 27, 2013

WIMBO WA KUHAMASISHA KASI YA MAENDELEO WAZINDULIWA KAGERA

MKOA wa Kagera umezindua wimbo maalumu utakaokuwa ukiimbwa wakati wa shughuli mbalimbali za kuhamasisha masuala ya maendeleo na  amani mkoani humo ambao umetungwa na msanii maarufu hapa nchini mwalimu John Mgango.

Wimbo huo umezinduliwa rasmi jana na mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabiani Massawe wakati wa kikao cha ushauri cha mkoa wa Kagera (RCC) kilichokuwa na lengo la kupitisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa huyo uliko katika manispaa ya Bukoba.

Akizundua wimbo huo awaagiza viongozi wahakikishe wimbo unahubiliwa  kwa kuwa utasaidia kuwaelimisha wanachi kuelewa mambo yanayokwamisha  maendele mkoani humo  na yanayochangia uvunjifu wa amani.

Mkuu huyo wa mkoa ameendelea kusema kuwa wimbo huo ulitafutiwa maneno mazuri yanayolenga dhana halisi ya amani na maendeleo ya mkoa wa Kagera, amesema mkoa wa Kagera una mkakati mkubwa wa kutokomeza vitendo vinavyokwamisha maendeleo na uvunjifu wa amani.


Kwa upande wake mtunzi wa wimbo huo John Mgango wakati wa uzinduzi huo amewaomba Watanzania wajiepushe na mkifarakano ili waweze kudumisha amani hapa nchini .

Massawe ni mmoja wa wanaharakati wa masuala ya maendeleo hapa nchini, mkoani Kagera amefanikiwa kubadili ya  mkitazamo ya wananchi mkoani humo hali ambayo imewawezesha kuondokana na masuala ya uvivu, majungu na masuala mengine yaliyokuwa yanakwamisha maendeleo mkoani Kagera.

MASSAWE AWALILIA WANANCHI WA KAGERA

SERIKALI imeombwa kufanya utaratibu wa kuwalipa fidia baadhi ya wananchi wa manispaa ya Bukoba iliyoko  mkoani Kagera walioondolewa kwenye makazi yao  ili  kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege uliko mjini  Bukoba.

Ombi hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe kwenye taarifa yake aliyoitoa kwa waziri wa uchukuzi Dr.Harrison Mwakyembe aliyekuwa mjini Bukoba kukagua maendeleo ya shughuli za upanuzi wa uwanja huo wa ndege.

Massawe amesema hadi sasa  ni wananchi 12 tu ambao wamelipwa fidia kwa ajili ya  kupisha upanuzi wa uwanja kati ya  41 waliofanyiwa tathimini, amesema wananchi hao mara kwa mara wamekuwa wakiandamana kudai haki yao kwenye ofisi yake.

Naye, mhandisi mshauri wa kampuni ya SSI inayosimamia ujenzi wa uwanja huo, Patrick Kain amemweleza waziri Mwakyembe sababu   zinazochangia kuchelewesha upanuzi wa uwanja huo wa ndege, ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na mvua zinazonyesha mara kwa mara katika mji huo na  ndege zinazoruka na kutua katika uwanja huo kutokuwa na ratiba maalumu.

Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa  maendeleo ya shughuli za upanuzi wa uwanja, waziri wa uchukuzi  Dr.Harrison Mwakyembe amesema kuwa ameridhishwa na shughuli zinazofanywa za upanuzi wa uwanja huo , amesema serikali itaweka utaratibu wa kuondoa vikwazo anavyokutana navyo mkandarasi vinavyopunguza  kasi yake  ya upanuzi wa uwanja huo ili uweze kumalizika kwa wakati.

Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 21 na unatarajia kumalizika mwezi agosti, mwaka huu, katika ziara hiyo Waziri Mwakyembe aliambata na naibu waziri wake Dr. Charles Tizeba.

Monday, March 25, 2013

JESHI LA POLISI KAGERA LASAMBATARISHA MTANDAO WA MAJAMBAZI

 Silaha mbalimbali zilizonaswa na jeshi la polisi baada ya kuua majambazi matano.
JESHI la polisi mkoani Kagera limefanikiwa kuwaua  watu watano wanatuhumiwa  kujihusisha na vitendo mbalimbali vya uharifu ambavyo ni pamoja wizi wa kutumia silaha na utekaji wa magari kwenye maeneo mbalimbali ya mapori yaliyoko mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa jeshi la polisi wa mkoa wa Kagera, Philip Kalangi amesema jeshi hilo limewaua watu hao  jana baada ya kukutana nao uso kwa uso katika eneo ya msitu wa Kalenge ulioko  wilayani Biharamulo wakati wakitoroka  kuelekea  wilaya ya Kakonko iliyoko mkoani Kigoma.

Anasema watuhumiwa hao baada ya kukutana na askari wa jeshi hilo walianza kurusha risasi ovyo kwa lengo la kujiami, Kalangi amesema pamoja na kurusha risasi hizo  askari hao walifanikiwa kuwazidi nguvu ambapo watuhumiwa wengine walilazimika kukimbilia maporini, watuhumiwa hao walikuwa  na  silaha mbili aina ya SMG,  risasi 35, magazine 2 na simu za mkononi nne, vyote ambavyo viko mikononi mwa jeshi hilo.


Kalangi  amesema waliouwawa walikuwa wakisakwa na jeshi la polisi kwa tuhuma ya kuhusika na tukio la utekaji wa magari manne  uliofanyika  hivi karibuni kwenye maeneo ya Nyamagala yaliyoko Rusaunga wilayani Biharamulo, amesema marehemu walipopekuliwa walikutwa na vitambulisho  vinaonyesha kuwa ni raia wa nchi jirani ya Burundi.

Ametoa wito kwa  wananchi waendelee kushirikiana na jeshi hilo ili liweze kupambana na vitendo vya uharifu ambavyo vinahatarisha amani ndani ya jamii kwa urahisi zaidi,amewaomba wananchi wamtolee taarifa mtu yoyote wanayemtilia mashaka.

MADIWANI WA HALMASHAURI YA MANISPAA YA BUKOBA WAENDELEA KUPINGANA NA MEYA ANATORY AMANI

 Mstahiki Meya wa manispaa ya Bukoba, Anatory Amani (kulia) ambaye madiwani wanataka ang,atuke, kushoto ni kaimu mkurugenzi mtendaji wa manispaa hiyo, Robert Kwela.
 Baadhi ya madiwani kabla ya kususia kikao wakipinga kuburuzwa na meya ambaye anadaiwa kutoa maamuzi kulingana na matakwa yake.
 Baadhi ya watendaji wa manispaa hiyo na wageni waalikwa walioudhuria kikao cha baraza la madiwani ambacho kilisusiwa.

Hali ya ukumbi baada ya madiwani kususia kikao, viti vinaonekana vikiwa wazi.

MANISPAA YA BUKOBA MAMBO YAENDELEA KUWAKA MOTO

BAADHI ya madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba wamegomea kikao cha baraza hilo na kutoka nje ya ukumbi wa mkutano baada ya kutokea malumbano makali kati yao na  mstahiki Meya wa manispaa hiyo Anatory Amani.


Hicho kilikuwa kikao cha kawaida cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo cha kujadili masuala ya mbalimbali yakiwemo ya  utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupokea taarifa za kamati, kilifanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya manispaa hiyo.


Mgogoro  ulianza baada ya madiwani  kuanza kuhoji  baadhi ya vipengele vya muhtasari wa kikao cha baraza la madiwani kilichopita kabla ya kuuthibitisha, wamedai kwamba katika kikao hicho kilichopita kuwa hawakukubaliana kurasimisha madaraka kwa kamati ya fedha na uchumi ili ifanye mchakato wa  kukopa fedha zaidi ya shilingi milioni 450 kwa ajili ya  kuwalipa wadeni.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti  madiwani hao wamesema katika kikao kilichopita hawakutoa Baraka kwa kamati ya fedha na uchumi kufanya mchakato kukopa fedha zaidi ya shjlingi milioni 200 toka  benki ya rasilimali nchini (TIB) kwa ajili ya kuilipa kampuni ya OGM itakayosimamia ujenzi wa soko jipya la Bukoba  na shilingi zaidi ya milioni 250 kwa ajili ya ajili ya kuandaa maeneo mbadala yatakayotumiwa wafanyabiashara watakaopisha ujenzi wa soko jipya la Bukoba. .


Madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Bukoba kila mara wamekuwa wakidai kuwa hawana imani na Meya Amani, kila mara wamekuwa wakimtaka aachachie ngazi kufuatia tuhuma mbalimbali wanazozielekeza kwake, madiwani wanamtuhumu diwani kuwa anaingia mikataba ya miradi mbalimbali ya maendeleo kinyemela, miradi anayodai meya ameiingia kinyemela kuwa ni pamoja na ujenzi wa soko jipya la Bukoba, upimaji wa viwanja 5,000 na ujenzi wa standi kuu ya mabasi.

Thursday, March 21, 2013

BALOZI WA TANZANIA NCHINI UBELGIJI ATOA MWALIKOMhe. Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Balozi wa Tanzania Ubelgiji, Uholanzi, Luxembourg na Jumuiya ya Ulaya anayo furaha kuwaalika Watanzania wote wanaoishi katika nchi za Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg kushiriki Tamasha la Filamu za Afrika ambalo litakuwa na siku mbili maalum za kuonyesha Filamu za Kitanzania. Filamu ya Kitanzania inayojulikana kwa jina la “A Teachers Country” itaonyeshwa  tarehe 29/03/2013 katika ukumbi wa sinema wa KINEPOLIS, Bondgenotenlaan 145, Leuven kuanzia saa mbili usiku. Aidha, tarehe 30/03/2013 Filamu za Kitanzania zinazojulikana kwa majina ya  “ The Road to Sainthood na Mwalimu: The Legacy of Julius Kambarage Nyerere”  zitaonyeshwa katika ukumbi wa Museum M, Leuven, Ubelgiji kuanzia saa 5.30 Asubuhi. Mhe. Madaraka Nyerere atakuwa mgeni rasmi.
Wote mnakaribishwa kuja kushiriki katika Tamasha la Filamu za Kitanzania.

Imetolewa na Dr. Diodorus Buberwa Kamala
Balozi wa Tanzania – BENELUX
21/03/2013

Dr. Kamala aendele kuinadi Tanzania

Balozi wa Tanzania katika nchi za Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg Balozi Dkt. Diodorus B Kamala akiwa na Rais wa Mahakama ya Dunia ya Haki (ICJ) H.E Peter Tomka. Balozi Kamala alienda alienda ofisini kwa Rais wa ICJ kwa nia ya kujitambulisha rasmi. Balozi Kamala anaratibu mahusiano ya Tanzania na mahakama ya ICJ.

Tuesday, March 19, 2013

WAZIRI MWAKYEMBE MKOANI KAGERA

 Waziri wa uchukuzi Harrison Mwakyembe (katikati) akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba, kulia Charles Kizeba naibu wake na kushoto, Seif Hussein afisa anayeshughulikia masuala ya miundombinu mkoani Kagera.
 Mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu Fabian Massawe akitoa maelezo kwa waziri Mwakyembe.
 Waziri Mwakyembe akiongea na mkuu wa mkoa wa Kagera alimuahidi kushughulikia malalamiko ya wananchi wanaodai fidia ambao waliondolewa kwenye maeneo yao kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba. Waziri Mwakyembe akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali baada ya kupata taarifa za upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba.
Waziri Mwakyembe akikagua uwanja.

KIKAO CHA KUJADILI CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WAFANYABIASHARA WANAOSAFIRISHA BIDHAA NJE YA NCHI

 Baadhi ya wajumbe wa kikao cha kujadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi kilichoandaliwa na wizara ya biashara na viwanda, kilifanyika kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Kagera.

 Wajumbe wengine.
 Fikir Kisimba afisa biashara mkoani Kagera akiongea wakati wa kikao hicho.

Naibu katibu mkuu wa wizara ya viwanda na biashara Shabaan Mwinjaka akiongea wakati wa kikao hicho, aliwaeleza wafanyabiasha kuwa serikali itahakikisha inaondoa vikwazo wanavyokumbana nao wafanyabiashara wanaposafirisha mizigo.

Monday, March 18, 2013

RAIS AKIPOKEA UJUMBE MAALUMU TOKA BOTSWANA


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Botswana uliowasilishwa na  Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi hiyo Mhe Pandu Skelemi
leo Ikulu jijini Dar es salaam.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisoma ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Botswana uliowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi hiyo Mhe Pandu Skelemi
leo Ikulu jijini Dar es salaam.

Dr. KAMALA APOKEWA NCHINI UHOLANZI

Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala akikagua gwaride la heshima siku alipowasilisha Hati za Utambulisho kwa Mtukufu Malkia Beatrix wa Uholanzi.

Saturday, March 16, 2013

KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI MKOA WA KAGERA

 Mwenyekiti wa halnashauri ya wilaya ya Misenyi, William Katunzi alikuwa miongoni mwa walioudhuria kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa kagera.
 Baadhi ya wakuu wa wilaya mkoani kagera.
 Kanali mstaafu Issa Njiku mkuu wa wilaya ya Misenyi,anayefuata ni mkuu wa wilaya ya Bukoba , Bi. Ziporah Pangani.
 Kutoka kushoto ni mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Kagera,Bi.Costancia Buhiye, Kanali mstaafu Fabian Massawe mkuu wa mkoa wa Kagera, na katibu tawala wa mkoa wa Kagera, Nassor Mnambila.
 Massawe akihutubia.

Thursday, March 14, 2013

WAZIRI MKUU PINDA MKOANI ARUSHA

Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akihutubia katika kilele cha sherehe za siku ya figo duniani kwenye viwanja vya hospitali ya AICC mjini Arusha Machi 14, 2012.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA UFUNGUZI RASMI WA JENGO LA KITIVO CHA SAYANSI KATIKA CHUO KIKUU CHA WAISLAMU CHA MOROGORO (MUM),

Mzee Kitwana Suleiman Kondo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF);
Mheshimiwa Joel Bendera, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;
Mama Mwantumu Malale, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro;
Profesa Hamza Mustafa Njozi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro;
Viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na Jumuiya mliohudhuria;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Niruhusuni niungane na wenzangu walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa.  Nakushukuru sana Mama Mwantumu Malale, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro na viongozi wenzako kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya ufunguzi wa jengo la Kitivo cha Sayansi katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro. Mmenipa heshima kubwa ya kuwa sehemu ya historia ya Chuo hiki.  Kwa kweli, nimefarijika sana kuona Chuo chetu kinazidi kupata mafanikio ya kutia moyo hasa ukizingatia ukweli kwamba kina muda mfupi tu tangu kuanzishwa kwake.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Natoa pongezi nyingi kwako, Makamu Mkuu wa Chuo na wale wote walioshiriki kubuni wazo la kuwa na jengo la Kitivo cha Sayansi na kufanikisha ujenzi wake.  Juhudi zao na moyo wao wa kupenda maendeleo ndio umetufanya sisi kujumuika hapa leo kushuhudia mafanikio haya. Hakika ni jambo la kujivunia. Pia, nawapongeza sana Wajenzi na Mhandisi Mshauri kwa kazi nzuri waliyofanya ya ujenzi wa jengo hili.  Sote tunaliona jengo lilivyojengwa vizuri na kwa namna yake linapendezesha mandhari ya Chuo. 
Kwa namna ya pekee napenda kwa niaba yenu nitoe shukrani zangu za moyoni kwa taasisi ya Al-Barakah kwa kufadhili ujenzi wa jengo hili.  Asanteni sana kwa ukarimu wenu na upendo mkubwa mliouonesha kwa nchi yetu na watu wake. Naomba taasisi nyingine na watu binafsi waige mfano huu mzuri wa kusaidia miradi mbalimbali inayonufaisha jamii.  Tukumbuke ule msemo wa wahenga kuwa “kutoa ni moyo, usambe si utajiri”.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Mabibi na Mabwana;
Kwa miaka mingi madhehebu ya dini  na mashirika ya dini yamekuwa washirika muhimu sana wa Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.  Yamekuwa yanajihusisha na kutoa huduma kwa jamii kama vile afya, elimu na nyinginezo. Kwa ajili hiyo watu wengi sana nchini wamenufaika na wanaendelea kunufaika na huduma zinazotolewa na mashirika ya dini.
Kwa miaka mingi  mashirika na  taasisi za madhehebu ya dini ya Kikristo ndiyo yaliyokuwa yakionekana kutoa huduma hizo. Kwa upande wa Waislamu, ukiacha Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan, mchango umekuwa mdogo sana. Ni jambo la faraja kubwa kuona Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF) ikionyesha njia.  Kwa kumiliki na kuendesha Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro kwa ufanisi, MDF inatoa mchango muhimu katika kuendeleza elimu ya juu na maendeleo nchini.  Idadi kubwa ya wanafunzi waliofuzu masomo yao na waliopo katika Chuo hiki tangu kilipoanzishwa mwaka 2005 ni ushahidi tosha wa kazi nzuri inayofanywa na MDF.  Hongereni sana.  Tunawaombea kwa Mola mpate mafanikio makubwa zaidi miaka ya usoni kwa upande wa elimu na huduma nyingine muhimu.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Katika kipindi cha miaka saba sasa, Serikali yetu imeongeza sana uwekezaji katika upanuzi wa elimu  tangu ya awali hadi elimu ya juu.  Tumeamua kufanya hivyo kwa sababu vijana wengi waliokuwa wanastahili kupata elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu walikuwa hawapati. Tanzania ni kubwa kuliko Kenya na Uganda kwa eneo na idadi ya watu lakini ndiyo tuliokuwa na idadi ndogo ya wanafunzi kwa ngazi zote hizo.  Kwa mfano, mwaka 2005 idadi ya wanafunzi waliokuwa Chuo Kikuu nchini Kenya ilikuwa 108,407, Uganda 88,360 na kwa baadhi ya nchi za SADC kama vile Afrika Kusini idadi hiyo ilikuwa 717,973. Wakati wenzetu wakiwa na idadi hiyo, sisi tulikuwa na wanafunzi 40,719 tu katika vyuo vikuu nchini.  Hali ilikuwa hivyo pia kwa elimu ya sekondari.  Kenya ilikuwa na wanafunzi 925,341, Uganda 619,519 na Afrika Kusini 4,186,882 wakati Tanzania ilikuwa na wanafunzi 524,325 tu waliokuwa katika shule za sekondari.
Tuliona hali hii haikubaliki hivyo tukaamua hatuwezi kuiacha iendelee.  Tukaamua kudhibiti. Tukachukua hatua tulizochukua za kupanua elimu katika ngazi zote.  Matokeo ya uamuzi huo ni kwamba vijana wanaopata fursa ya kupata elimu katika ngazi zote wamekuwa wengi kuliko wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu, tumewafikia na kuwapita majirani zetu. Kazi kubwa tunayoendelea nayo sasa ni kuwekeza katika kuimarisha ubora wa elimu waipatayo vijana wetu kwa kuongeza walimu, vifaa vya kufundishia, vitabu na huduma nyinginezo. Inshallah hata kwa dhamira yetu, hii njema Mola atatuwezesha. Mwanzo mgumu lakini hatma itakuwa nzuri.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Kufuatia juhudi hizo, idadi ya wanafunzi waliopo kwenye vyuo vikuu nchini imeongezeka sana, kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi wanafunzi 166,484 mwaka 2012. Kwa upande wa sekondari mwaka 2011 tulikuwa na wanafunzi milioni 1.79 na wenzetu wa Kenya walikuwa na wanafunzi milioni 1.77. Haya ni mafanikio makubwa.
Serikali itaendelea kuwekeza  kwenye upanuzi wa fursa za elimu na ubora wake. Hata hivyo ushiriki wa wadau wengine kuunga mkono juhudi za serikali ni jambo muhimu sana.  Tumeweka  mazingira mazuri kwa wadau hao kufanya hivyo na mafanikio yanaonekana wazi. Kama nilivyokwishasema awali, mashirika ya dini yamekuwa wadau wa kutumainiwa na mchango wao uko wazi. Unajieleza wenyewe. Kwa mfano, katika vyuo vikuu 49 vilivyopo nchini, vinavyomilikiwa na umma ni 14 tu. Vyuo vikuu 24 vinamilikiwa na mashirika ya dini na 11 na sekta binafsi.


Ndugu Mkuu wa Chuo;
Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa na muhimu unaotolewa na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na mashirika ya dini na sekta binafsi.  Ninyi mmekuwa washirika wazuri na wa uhakika katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu katika nchi yetu.  Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nanyi ili kuwawezesha vijana na Watanzania wengi zaidi waweze kupata elimu. Uamuzi wa kufanya utaratibu wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu uhusishe wanafunzi wa vyuo visivyokuwa vya umma ni moja ya mambo mengi muhimu yanayofanywa na Serikali kuthibitisha usemi wangu huo.  
Tulipoingia madarakani mwaka 2005 tulifanya mambo mawili muhimu kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.  Kwanza uamuzi kwamba, mikopo itolewe kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma na vile visivyokuwa vya serikali. Kabla ya hapo ilihusu vyuo vya umma pekee. Pili kwamba, kila mwaka tuongeze fedha zinazotengwa  kwa ajili ya Mfuko huo ili idadi ya wanafunzi wanaonufaika iongezeke. Tulikuta Mfuko ukiwa na  shillingi billioni 56.1 unanufaisha wanafunzi 16,345 mwaka 2005. Tukaongeza kila mwaka na katika mwaka huu wa fedha (2012/13) tumetenga shillingi bilioni 345 zinazowanufaisha wanafunzi 98,772.
Tutaendelea kuongeza fedha katika Mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na hata ifikie siku moja tuweze kuwakopesha wote bila ya kujali sifa ya uwezo wa wazazi au walezi kulipa ada.  Kwa kasi tuliyonayo na kwa jinsi tunavyozidi kufanikiwa katika kukusanya mapato ya serikali, naamini miaka michache ijayo tunaweza kufikia lengo hilo. Nawasihi Bodi ya Mikopo iwekeze katika  kuimarisha uwezo wa kuwafuatilia waliokopeshwa kulipa mikopo waliyopewa. Matamanio yangu ni kuwa fedha zilizotolewa zizunguke ili tupunguze kiasi kinachotolewa na bajeti ya serikali kila mwaka.   
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Mabibi na Mabwana;
Niruhusuni nitumie nafasi hii kukupongeza wewe Mkuu wa Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo, Wahadhiri  na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu hiki  kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo ya kuendeleza na kuboresha Chuo. Tumeshuhudia ujenzi wa jengo nililolifungua leo. Tumeona mafanikio kwa upande wa ongezeko la idadi ya wanafunzi, walimu, wafanyakazi na fani zinazofundishwa katika kipindi hiki kifupi cha uhai wa Chuo hiki.
Nimefurahishwa na kufarijika sana  kusikia kuwa ubora wa elimu inayotolewa hapa chuoni ni jambo linalopewa kipaumbele cha kwanza.  Jambo hili ni muhimu sana kulisisitiza kwani tunataka wahitimu wa Chuo hiki wafanane na wahitimu wa Chuo chochote kizuri nchini na hata duniani.  Ningependa kuona wahitimu wa Chuo hiki wanagombewa katika soko la ajira.  Hili ni jambo linalowezekana.  Kinachotakiwa  ni uamuzi wa Baraza na Seneti kuwa iwe hivyo na kuchukua hatua zipasazo.  Sina shaka kuwa mnaweza kufanya hivyo.  Hakika mnaweza, na sote kwa umoja wetu tunaweza.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Nimefurahi sana, pia, kusikia kuwa Chuo kinatoa mafunzo ya ualimu. Bila ya shaka mnaelewa kwa nini nafurahi. Tuna uhaba mkubwa wa walimu nchini hivyo Chuo cho chote kinachotoa mafunzo ya ualimu hunifurahisha.  Endeleeni kuimarisha mafunzo hayo ili Chuo chenu kitambulike na kukubalika nchini kwa sifa ya kutoa walimu wazuri.  Walimu wa kutoka Chuo hiki wawe wale wanaojua vyema masomo wanayofundisha, mahiri kufundisha na waadilifu.  Naomba pia mtoe kipaumbele cha juu kwa mafunzo ya ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati.  Mkifanya hivyo, mtakuwa mnatoa mchango mkubwa katika jitihada za kupunguza uhaba wa walimu wa masomo hayo nchini.  Naamini kitendo cha kuzindua Jengo la Kitivo cha Sayansi, kilichofanyika muda mfupi uliopita kinatoa matumaini ya Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro kuchangia katika jitihada za kupunguza pengo la walimu wa sayansi nchini.  
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Nimewasikia mkieleza kwa ufasaha changamoto kubwa na ndogo ambazo Chuo inakabiliana nazo.  Nawapongeza kwa dhati, wewe na viongozi wenzako kwa ubunifu wenu na hatua mnazochukua kuzikabili changamoto hizo.  Nawaahidi msaada na ushirikiano wangu na wa serikali kwa yale yaliyoko kwenye uwezo wangu na wa serikali katika kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zinazowakabili.
Nawapongeza kwa uamuzi wenu wa kutafuta vyuo vikuu rafiki vilivyoko katika nchi mbalimbali duniani mnavyoweza kushirikiana navyo.  Endeleeni kufanya hivyo kwani vyuo vikuu vingi duniani hufanya hivyo.  Hamtakuwa wa kwanza na wala hamtakuwa mnafanya jambo la kustaajabisha. Mnaweza,        mkipenda, kuwaomba Mabalozi wetu waliopo katika nchi mbalimbali duniani wawasaidie. Ni wajibu wao kufanya hivyo kwani kusaidia kusukuma maendeleo ya hapa nchini kutoka huko waliko ndilo jukumu lao la msingi. Vile vile, nimefurahishwa na mipango yenu ya baadaye ya kuwa na matawi katika mikoa mbalimbali nchini.  Hongereni kwa uamuzi wenu wa busara. Lazima Chuo kitanuke kwa maana ya kuwa kikubwa zaidi, makao makuu na kwa kuwa na vyuo vishiriki na shule au  vitivo sehemu mbalimbali nchini.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Kazi iliyo mbele yenu ni kubwa, hivyo ni vyema kuweka mikakati mizuri na mipango thabiti ya utekelezaji na ufuatiliaji wa dhamira yenu hiyo njema.  Rai yangu kwenu ni kuwaomba muwe wabunifu zaidi hasa katika kutafuta vyanzo vingine vya mapato vitakavyosaidia Chuo kujiendesha bila kutegemea ada peke yake.  Chuo kiangalie uwezekano wa kufanya shughuli zitakazowaingizia mapato kama vile kufanya shughuli za kutoa ushauri. Pia muangalie uwezekano wa kuwekeza wenyewe kwenye miradi ya kiuchumi au kwa kushirikiana na wawekezaji katika baadhi ya maeneo.
Kuhusu nafasi mbili za ufadhili nilizopewa na Chuo kikuu cha Tun Abdul Razak cha Malaysia, nitafuatilia kujua  kilichoendelea na kinachoendelea. Je, nafasi hizo bado zipo?  Zikiwepo, nitawasiliana na wahusika waangalie uwezekano wa kuwapeni. Kama zimeshagawiwa basi tusubiri safari ijayo. Kwa  masuala ya ardhi na maombi mengine nimeyasikia, yaleteni tuangalie namna ya kusaidiana. 
Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo, na
Wafanyakazi wote wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;
           Napenda kuwakumbusha kuwa mnayo dhamana kubwa na wajibu mkubwa na wa kihistoria. Ule ukweli kwamba ni mara ya kwanza kwa Taasisi ya Waislamu wazawa kuwa na Chuo Kikuu inawapeni wajibu maalum wa kuhakikisha Chuo kinafanikiwa. Ni mtihani na changamoto ya aina yake kuthibitisha kuwa Waislamu nao wanaweza kuwa na Chuo kizuri na chenye kutoa elimu ya ubora wa hali ya juu.  Kwa sababu hiyo hamna budi kuhakikisha kuwa mna mipango mizuri ya kujenga Chuo cha hadhi na ubora wa hali ya juu.  Ihakikishwe kuwa mipango hiyo inatekelezwa kwa ukamilifu. 
           Aidha jumuiya yote inao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, maarifa na weledi ili dhima hiyo ya Chuo iweze kutimizwa kwa ukamilifu. Timizeni wajibu wenu ipasavyo ili jina la Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro likue haraka. Sifa yake isambae na kuvuma kote nchini. Chuo kifanye vizuri ili wanafunzi waone fahari kuwa wahitimu wa Chuo hiki. Chuo ambacho, wazazi wapende kuleta vijana wao kuja kusoma hapa. Kwa jinsi Mkuu wa Chuo alivyoeleza, mimi nina imani mnaweza, fanyeni kweli.


Ndugu Wanafunzi wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;
Naomba wote muone fahari ya kuwa wanafunzi katika Chuo cha kihistoria hapa nchini.  Nawasihi mjitume kwa kadri ya uwezo na vipaji mlivyopewa na Mwenyezi Mungu mfanikishe kile kilichowaleta.  Jifunzeni kwa bidii mfaulu vizuri ili mkihitimu muwe kielelezo kizuri cha mafanikio na ubora wa  Chuo  Kikuu Cha Waislamu cha Morogoro.  Muwe Mabalozi na kioo cha ufanisi wa Chuo hiki. Nawasihi mjiepushe na mambo yatakayowapunguzia muda au kuwaondoa katika shughuli ya msingi iliyowaleta hapa ya kujifunza mpate digrii katika fani mliyochagua mwenyewe kuisomea.  Vishawishi ni vingi na wapo watu wengi wanaopanga kuwashawishi mtumie muda wenu adhimu kufanya wanayoyataka wao ambayo mkishiriki huwatoa kwenye malengo na kutekeleza yao. Mambo ya dunia ya nje ya Chuo ni mengi huna budi kutambua lipi ufanye na lipi usifanye na kwa wakati gani! 
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu ni mtu mzima, si mtoto. Lazima ujue kuwa unawajibika kwa kila unaloamua na kutenda.  Amua kuwajibika vizuri. Fikiri kabla ya kutenda, changanua lipi ni lipi kabla ya kufanya uamuzi wa kile unachotaka kufanya.  Wakati wote uongozwe na busara na hekima na siyo jazba na ushabiki wa matakwa ya kundi.  Kama ni jema fanya na kama si jema usifanye.  Kwanza tambua wewe ni nani na uko hapa kwa ajili gani. Lazima ujue kuwa hatma ya yote uko peke yako.  Utafaulu au kufeli wewe.  Utapata shahada wewe na si mtu mwingine.  Hakuna ubia wa kufaulu au kufeli au kiwango cha kufaulu. It will always remain personal. Katika masomo unanufaika wewe.  Shirikiana na wengi lakini usisahau kujali maslahi yako.  Maslahi ya wengi yasiyojumuisha yako, yahoji vizuri kabla ya kuamua kushiriki au kufanya. Vinginevyo labda kama umeamua kujitoa muhanga, uwe shujaa. Hata kwa hilo, sijui utakuwa shujaa wa nani.
Mabibi na Mabwana;
Kabla ya kumaliza napenda kutambua na kumshukuru Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa na viongozi wa MDF kwa juhudi zao za pamoja zilizowezesha Chuo hiki kuwepo.  Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru wananchi wanaokizunguka Chuo kwa ujirani mwema na wakazi wa Morogoro kwa ujumla kwa kukipokea vizuri na kuishi na wanajumuiya wa Chuo hiki kwa upendo mkubwa. Naomba muendelee na moyo na ushirikiano huo.
Baada ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunialika. Nawatakia kila la heri na mafanikio tele.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

RAIS KIKWETE AZINDUA JENGO LA CHUO KIKUU Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa  na mmoja wa wahadhiri Profesa Juma Mikidadi Mtupa (aliyeketi) Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Mama Mwantumu Malale, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Hamza Mustafa Njozi na wadau baada ya kuzindua rasmi jengo la Kitivo cha Sayansi la Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro leo Machi 14, 2013 mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Mama Mwantumu Malale. Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipunga mkono kuaga wanafunzi na wafanyakazi baada ya kuzindua rasmi jengo la Kitivo cha Sayansi la Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro leo Machi 14, 2013 mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Mama Mwantumu Malale.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifunua pazia kuzindua rasmi jengo la Kitivo cha Sayansi la Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro leo Machi 14, 2013 mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Mama Mwantumu Malale.