Saturday, February 16, 2013

SOMO LA DINI NA MAADILI KUFUNDISHWA RASMI SHULENI NA VYUONI TANZANIA NZIMA



MIKOA ya Kagera na Kigoma imezindua rasmi mihtasari  ya  somo la Dini na Maadili litakalofundishwa kuanzia shule za awali, msingi sekondari hadi vyuo vikuu.

Mihtasari hiyo imezinduliwa  rasmi na UMAKA (Umoja wa Madhehebu Kagera) wakishirikiana na serikali baada ya mihtasari hiyo kupitishwa rasmi na Kamishina wa Elimu ili isambazwe katika shule zote tayari kwa kutumika kufundishia wanafunzi katika ngazi mbalimbali.

Somo la Dini na Maadili limerasimishwa rasmi kufundishwa shuleni na vyuoni baada ya UMAKA kuona umuhimu wa kuwa na mihtasari ambayo ni rasmi na inayotambuliwa na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili itumike kufundishia watoto pia na kutahiniwa kama masomo mengine.

Umoja wa Madhehebu Kagera  (UMAKA) ulianzisha mchakato wa kuandaa mihtasari ya somo la Dini na  Maadili  wakishirikiana na serikali ili somo hilo liwe na mihtasari inayofanana katika kufundishia wanafunzi kuliko hapo awali ambapo somo hilo halikuwa na mihtasari ya kufundishia.

Kupitia somo la Dini na Maadili, wanafunzi  watafunzwa maadili mema ya kupendana na kuwapenda watanzania wenzao, kujenga jamii yenye kuwajibika na kumcha Mwenyezi Mungu bila kujali tofauti za ki-imani kwao, pia kulelewa na kukua katika malezi ya kufuata sheria na utawala bora.

Serikali katika kuboresha utumiaji wa Mihtasri mipya ya somo la Dini na Maadili imeagiza somo hilo likaguliwe na wakaguzi wa serikali pamoja na walimu wakuu wa shule kama masomo mengine na kutahiniwa katika ngazi zote hadi ile ya taifa.

Pia katika kuona umuhimu wa somo la Dini na Maadili kufundishwa shuleni, serikali imeamua mihtasari ya somo hilo itumike Tanzania nzima badala ya Mikoa ya Kagera na Kigoma walioshirikiana na serikali kuandaa mihtasari hiyo  ili wanafunzi wote wa Tanzania wafunzwe dini na maadili ya kitanzania.

UMAKA ilianzishwa miaka ya 1980 ikiwa na lengo la kushirikiana na Serikali na kushauri masuala mbalimbali yahusuyo maadili, amani, usalama na maendeleo ya jamii ya watanzania. UMAKA inajumuisha  Balaza la Maaskofu Tanzania (TEC),  Balaza la Waislam Tanzania (BAKWATA), na Baraza la Wakristo Tanzania (CCT).

No comments:

Post a Comment