Tuesday, November 06, 2012

KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MULEBA

 Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Muleba wakisikiliza kwa makini maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu, Fabian Massawe.
 

Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imepewa  miezi mitatu kujisafisha yenyewe na kuwachukulia hatua watendaji wote waliohusika  na ufujaji wa fedha za serikali, kutozingatia kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao kwa wananchi wa Wilaya ya Muleba.
Muda wa miezi mitatu  ulitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kanali Mstaafu Fabian I. Masswe alipokuwa mgeni rasmi katika kikao cha balaza la Madiwani (Full Council) kilichofanyika siku ya Ijumaa tarehe 2/11/2012 wakati alipowasilisha ripoti maalum.
Mhe. Massawe alitoa muda huo baada ya kuwasilisha ripoti ya ukaguzi maalumu mbele ya Madiwani uliofanyika mwezi Agosti mpaka Septemba 2011 kwenye halmashauri hiyo ambapo ukaguzi huo uliombwa na Madiwani wenyewe kuwa ufanyike baada ya kutordhika na mwenendo wa Halmashauri yao.
Ripoti ya ukaguzi maalum uliofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hazina pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera ilibainisha kuwa vitabu 133 vya kukusanyia ushuru havijulikani  vilipo, Halimashauri haijui vitabu hivyo viko wapi.
Pia ripoti hiyo ilibainisha kuwa baadhi ya watendaji wa kata na vijiji kuwa na vitabu mara mbili ambavyo wanavitumia kukusanyia  ushuru  wa halmashauri jambo ambalo linaikosesha halmashauri hiyo kutopata mapato kutokana  na watendaji hao kutowasilisha kabisa au kuwasilisha  mapato kidogo kwenye Halmashauri tofauti na wanavyokusanya.
Vile vile ripoti maalum ya ukaguzi ilibainisha sehemu kubwa ya malipo kufanyika bila kufuata utaratibu wa kulipa fedha za serikali ambapo nyaraka za ulipaji hazikuonekana, pia mlipwaji hajulikani ni nani na fedha zilizolipwa zililipwa bila kuidhishwa na serikali.
Aidha ripoti hiyo pia ilibaini udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, usimamizi wa miradi ya maendeleo, Halmashauri kufanya manunuzi makubwa kwa kutumia masurufu, Usimamizi mbovu wa mali za Halmashauri na upotevu wa mali za Halmashauri katika ngazi za vijiji.
Mkuu wa Mkoa aliiagiza Halmashauri pamoja na Madiwani wake kuwabaini waliohusika na kuwachukulia hatua za kinidhamu ndani ya miezi mitatu na taarifa kuwasilishwa kwake.Baadhi ya Maafisa wanaohusishwa na tuhuma hizo ni pamoja na Mhandisi wa ujenzi na Mratibu wa TASAF.
Wilaya ya Muleba imekuwa katika malumbano ya  kisiasa ya muda mrefu jambo ambalo linairudirudisha nyuma kimaendeleo huku miradi ya maendeleo ikishindwa kuteketelezeka kwa wakati kutokana na malumbano hayo jambo  alilokiri mbele ya kikao hicho mwenyekiti wa Halmashauri Bw. George Katomelo wakati wa kufungua kikao hicho cha balaza la Madiwani.

No comments:

Post a Comment