Tuesday, October 16, 2012

CHIZZA AONYESHA MAKEKE YAKE MKOANI KAGERA

WAZIRI wa ushirika, chakula na masoko Mhandisi Christopher Chizza amewahimiza viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika nchini kushikamana  ili waweze kuendeleza  na kuviimarisha vyama vya vyao badala ya kujenga dhana ya kuvididimiza.    

Mhandisi Chizza aliyasema hayo jana wakati wa kikao chake na viongozi wa serikali ya mkoa wa Kagera, uongozi wa chama cha ushirika Kagera (KCU) na waandishi wa habari kilichofanyika kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Kagera.

Katika kikao hicho alisema migongano  zinazojitokeza kati ya  baadhi  ya wanachama wanaounda vyama ushirika na waliopewa jukumu la kusimamia na kuongoza vyama vya ushirika kamwe haziwezi kuviimarisha na kuviendeleza vyama vya ushirika.

Alisema kuwa duniani kote migongano ndio huwa chanzo cha kudidimiza vyama vya ushirika, Chizza alisema ili vyama vya ushirika viweze kuimarika na kuendelea  ni lazima wana ushirika wapendane, waaminiane na waheshimiane, “hizi  ndio nguzo kuu zinazoimarisha ushirika”alisema kwa msisitizo.

“Ndugu zangu viongozi wa KCU ninapokea barua rundo zinazowatuhumu, nyingine zinazoelea masuala ya ubadhilifu na barua hizi zinaandikwa na wanaushirika wenu, ila taarifa mliyonipa ya utendaji wa kazi naiona iko wazi na inaelezea hali halisi ya utendaji kazi mzuri wa KCU, sasa sielewi hizi barua zinaashiria kitu gani” alisema kwa msangao.

Aliuagiza uongozi wa KCU kuwawajibisha watendaji ndani ya ushirika huo wanawaona wanajihusisha na masuala ya ubadhilifu wa mali ya wakulima, alisema yoyote wanayemuona anajihusisha na masuala ya ubadilifu wasiishie kumfukuza tu bali wamfikishe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa KCU, John Binunshu katika taarifa yake kwa waziri huyo aliiomba serikali isitoe vibali  vya kununua kahawa moja kwa moja toka kwa wakulima kwa  makampuni makubwa ambayo ununua kahawa inayakusanywa na vyama vya ushirika moja kwa moja mnadani.

Binunshu alisema kuwa hali ya serikali kutoa vibali kwa makampuni hayo makubwa inadhoofisha vyama vya ushirika kwa kuwa yanachangia mnada wa kahawa kuchelewa, alisema minada ya kahawa inapochelewa vyama vya ushirika vinakosa fedha za kuwalipa wakulima hivyo vinalazimika kununua kahawa kwa mkopo.

Akitoa ufafanuzi juu ya kwa nini baadhi ya wanunuzi wa kahawa wananunua kahawa kwa bei kubwa alisema, wanaonunua kahawa kwa bei kubwa ni wale wanaonunua kahawa bila kutumia minzani, aliendelea kuwa wanunuzi hao wananunua kahawa kwa ujazo badala ya kilo jambo ambalo linawapunja wakulima.

Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bi. Ziporah Pangani alikiri kuwepo kwa magendo ya kahawa, alisema kamati yake ya ulinzi na usalama inalishughulikia suala hilo, alimaliza kwa kusema kuwa kamati yake imeshakamata magari yaliyokuwa yanavusha kahawa kwa njia ya magendo na kufilisi kahawa hiyo.

No comments:

Post a Comment